ASKOFU SANGU AKITANGAZA KIGANGO CHA MWAMASHELE KUWA PAROKIA TEULE.

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amekitangaza Kigango cha Mtakatifu Yosefu Mwamashele kilichopo katika Parokia ya Wila wilayani Kushapu  Jimbo Katoliki Shinyanga  kuwa Parokia teule.

Askofu Sangu ametoa tamko hilo Jumatano tarehe 16.10.2024 wakati akijibu risala iliyosomwa  mbele yake baada ya adhimisho la Misa takatifu ya Kipaimara iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Theresia Wila.

"Katika risala yenu mmeomba Mwamashele  kwamba iwe Parokia teule basi mimi kwa mamlaka niliyopewa na Mama Kanisa natamka leo kwamba Mwamashele ni Parokia teule na ninawaomba waumini wote muungane nyote kwa pamoja kukamilisha miundo mbinu ili kweli siku moja nikija tena hapa namleta Padre kwa ajili ya kukaa pale"

Askofu Sangu amewataka waamini kushirikiana kwa pamoja kuboresha miundombinu ya Kigango hicho ili kuwezesha mchakato wa kukipa hadhi ya kuwa Parokia kamili.

Aidha Askofu Sangu amebainisha kuwa Parokia teule ya Mwamashele itaundwa na Vigango 16 ikiwemo Mwamashele yenyewe na Vigango vingine 14 vilivyopo ndani ya Parokia ya ya Mtakatifu Theresia Wila pamoja na Kigango kimoja kutoka Parokia ya Mhunze.

"Parokia teule itakuwa na Vigango vifuatavyo:-  Mwamashele yenyewe, Isagala , Igumila, Bubinza, Busungu, Lwagalalo, Mwamadulu, Lagana, Mihama, Idushi, Veledi, Mwamanota, Inolelo, Ngofila, Kalitu, Nyawa ambavyo vyote kwa saa viko katika Parokia ya Wila pamoja  na Ipojamitwe kutoka Parokia ya Mhunze itahamia huko "

Parokia teule ya Mtakatifu Yosefu Mwamashele ilianza kama kigango mwaka 1960 chini ya Parokia ya Wila ambayo kwa sasa ni Senta inayounganisha vigango  mbalimbali.

Previous Post Next Post