Ticker

6/recent/ticker-posts

ASKOFU SANGU KUJIANDIKISHA KWENYE ORODHA YA WAPIGA KURA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashsmu Liberatus Sangu, leo atajiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika nchini  kote Novemba 27 mwaka 2024.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Katibu wa Askofu Padre Richard Makoye, Askofu Sangu atakwenda kujiandikisha majira ya saa nane mchana kwenye kituo cha Shule ya Msingi Bugoyi mtaa wa Mbuyuni Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, mara baada ya ziara yake ya kichungaji katika Parokia ya Lubaga.

Tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, Askofu Sangu amekuwa akitumia ziara zake kuwahamasisha waamini na watanzania wote kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo ikiwemo kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili kuwapata viongozi wanaowataka na kwamba, uchaguzi huo una umuhimu mkubwa katika ustawi wa taifa.

Aidha, Askofu Sangu amekuwa akiwahimiza watanzania wenye sifa ikiwemo wanawake kujitokeza   kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ambazo ni pamoja  uenyekiti wa mtaa, kijiji na kitongoji.

Zoezi la uandikishaji katika daftari la orodha ya wapiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa linahitimishwa nchini kote leo Jumapili majira ya saa 12:00 Jioni, ambapo mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea utaendelea siku chache zijazo.

Tayari Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Serikari za Mitaa na tawala za mikoa (TAMISEMI) ametangaza ukomo wa madaraka kwa viongozi waliokuwa wakishikilia nafasi hizo mpaka pale watapochaguliwa wengine, na majukumu yao kwa muda yatakuwa chini ya watendaji wa mitaa na vijiji.

Post a Comment

0 Comments