BONANZA LA MICHEZO HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA LATOA UJUMBE KUHUSU UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2024, WANANCHI WAHAMASISHWA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAKAZI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, ametoa wito kwa wananchi wa Halmashauri hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili kupata haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Dkt. Kalekwa ametoa wito huo wakati wa bonanza la michezo ambalo limefanyika katika Stendi ya Mabasi ya Salawe, na kwamba lililenga kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi.

“Siku za kujiandikisha zimebaki chache, zoezi hili lilianza Oktoba 11 na litatamatika tarehe 20, naomba wananchi mjitokeze kwa wingi ili mtumie haki yenu ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo."amesema Dkt. Kalekwa

Bonanza hilo limevutia wakazi wengi wa Salawe na maeneo jirani, wakifurahia michezo mbalimbali kama kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na magunia, na ngoma za kitamaduni.

Michezo hiyo imeandaliwa kwa makusudi ya kuwasilisha ujumbe muhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la wakazi, ambapo viongozi wamesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu, ameungana na Dkt. Kalekwa kuwahimiza wananchi, hasa wale ambao bado hawajajiandikisha, kuhakikisha wanatumia muda uliosalia kujiandikisha.

 “Siku siyo rafiki, naomba wale ambao bado hawajajiandikisha wafanye hivyo ili wasikose fursa ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka," amesema Mhe. Buyugu.

Misalaba Media imezungumza na baadhi ya wananchi walioshiriki bonanza hilo, ambao wameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa jitihada zake za kuhamasisha ushiriki katika zoezi la kujiandikisha.

Wananchi hao wamesema kuwa wengi wao tayari wamejiandikisha na hawajakutana na changamoto yoyote katika mchakato huo.

Aidha, wananchi waliohudhuria bonanza wameeleza kufurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi wa Halmashauri na jamii, hali ambayo inachangia kuongeza mwamko wa wananchi kuhusu uchaguzi ujao.

Uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, utawahusisha wananchi katika kuchagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa pamoja na wajumbe.

 Zoezi hilo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii kwani litatoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao.

Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imeendelea kuweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha wananchi wote wanapata nafasi ya kujiandikisha kwa wakati, hatua ambayo inawawezesha kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.






Msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, akiendelea na zoezi la kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali katika bonanza hilo la michezo.

Msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, akiendelea na zoezi la kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali katika bonanza hilo la michezo.


Previous Post Next Post