DIWANI MSABILA MALALE ADAIWA KUMTWANGA NGUMI MWENZAKE KATA YA IBADAKULI

Diwani wa kata ya Ibadakuli Mhe. Msabila Malale upande wa kushoto, na Diwani wa viti maalum kata hiyo Mhe. Zuhura Waziri wa kwanza upande wa kulia.

Katika zoezi la uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Diwani wa Kata ya Ibadakuli, Bwana Msabila Malale Kulwa, anadaiwa kumshambulia Diwani mwenzake wa viti maalum, Bi Zuhura Waziri, mnamo Oktoba 23, 2024.

Tukio hilo linadaiwa kutokea katika kijiji cha Ibadakuli, wakati Bi Zuhura alikuwa akisimamia upigaji kura za maoni. Inadaiwa kuwa Bwana Msabila alimpiga makonde Diwani huyo, jambo lililosababisha majeraha usoni mwake na kumpeleka kulazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mashuhuda wanadai vurugu hizi zilitokana na tofauti za kisiasa na kutokuelewana kati ya madiwani hao wawili.

Misalaba Media imewasiliana na Diwani wa viti maalum, Mhe. Zuhura Waziri, ambaye amesema kuwa alitoka jana usiku katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga baada ya kulazwa kutokana na shambulio hilo, lakini hali yake ya kiafya bado siyo nzuri.

Pia Misalaba Media imemfatuta Diwani wa kata ya Ibadakuli Mhe. Msabila Malale ambaye amesema kwa sasa yupo nje ya Manispaa ya Shinyanga na hakutaka kulizungumzia suala hilo.

Tunaendelea kufuatilia kwa undani tukio hilo na tutaleta taarifa zaidi pindi zitakapopatikana.


Previous Post Next Post