Na Mapuli Kitina Misalaba
Katika jitihada za kuhakikisha wakazi wa Shinyanga
wanashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, zoezi la
uandikishaji wakazi limeanza rasmi tarehe 11 Oktoba na litarajiwa kumalizika
tarehe 20 Oktoba.
Uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti wa mtaa utafanyika
tarehe 27 Novemba, mwaka huu, huku wakazi wa kata ya Ngokolo wakihimizwa
kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo muhimu.
Akizungumza baada ya kujiandikisha katika kituo cha
Madaktari Bingwa kilichopo mtaa wa Majengo Mapya, Diwani wa kata ya Ngokolo,
Mhe. Victor Yessaya Mkwizu, ameonyesha hamasa kubwa kwa wananchi wa kata yake
kujiandikisha.
“Leo nimepata fursa ya kuja kujiandikisha kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti
wangu wa serikali ya mtaa, Tunajiandikisha kwenye daftari la makazi kwa ajili
ya kumchagua mwenyekiti wetu wa serikali ya mtaa, kwahiyo nawaomba wakazi wote
wajitokeze ili waweze kutimiza haki yao ya kidemokrasia.”amesema Mkwizu
Kata ya Ngokolo ina jumla ya mitaa saba, na kwa
mujibu wa Diwani Victor Mkwizu, ni muhimu wakazi wote wa mitaa hiyo wajitokeze
ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa mafanikio na uwazi.
“Niwaombe wakazi wote wa kata ya Ngokolo, kwenye mitaa yote saba,
mjitokeze kwa ajili ya kwenda kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili muweze
kumchagua mwenyekiti wa mtaa wenu,” amesema Mkwizu.
Diwani Mkwizu pia amefafanua kwamba kumekuwa na
mkanganyiko kwa baadhi ya wakazi kuhusu mchakato huu wa uandikishaji, ambapo
wengine wanadhani ni uandikishaji kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amefafanua tofauti kati ya zoezi hilo la sasa na
uandikishaji wa kudumu wa wapiga kura wa Tume ya Uchaguzi.
“Hili zoezi tunalofanya sasa ni tofauti na uandikishaji wa wapiga kura wa
mwaka 2025. Hili ni kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya
kuchagua viongozi wa mitaa yetu. Kwa hiyo, nawasihi wananchi wote wajitokeze
kwa wingi kushiriki zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya mtaa na kata yetu kwa
ujumla,” amesema Diwani Mkwizu.
Zoezi hilo la uandikishaji linaendelea kwa siku kumi,
likihitimishwa tarehe 20 Oktoba, likiwa na lengo la kuwezesha uchaguzi huru na
wa haki, ambapo viongozi wa mitaa watakaochaguliwa watakuwa na jukumu kubwa la
kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Wakazi wa Shinyanga, hususan kutoka kata ya Ngokolo, wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wanaweka viongozi wanaowaamini na watakaosimamia vyema maendeleo ya jamii zao.
Diwani wa kata ya Ngokolo, Mhe. Victor Yessaya Mkwizu, akijiandikisha kwenye daftari la wakazi.