FLAVIANA MATATA FOUNDATION WAKABIDHI CHOO CHA WASICHANA SHULE YA SEKONDARI MASEKELO,CHENYE CHUMBA MAALUMU CHA KUJISTIRI HEDHI

 




RC Macha ataka faragha kujistiri hedhi


TAASISI ya Flaviana Matata Foundation,imekabidhi Serikali choo cha kisasa cha wasichana katika shule ya Sekondari Masekelo Manispaa ya Shinyanga, chenye matundu 12 kikiwa na chumba maalumu cha kujistiri hedhi.

Hafla hiyo ya makabidhiano na uzinduzi wa chooo hicho, imefanyika leo Octoba 3,2024 katika shule ya Sekondari Masekelo,huku mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Macha ameipongeza Taasisi hiyo kwa kusaidia wanafunzi wa kike kukuza taaluma yao, kwa kuwajengea choo chenye chumba maalumu cha kujistiri hedhi ili wasikose vipindi vya masomo wanapokuwa katika siku zao, na kwamba suala la hedhi lina hitaji faragha.

“Mwanafunzi wa kike anahitaji faragha kujistiri hedhi, na huo ndiyo utamaduni na heshima ya binadamu kwa kulinda utu wao, na hata kuzihifadhi taulo za kike ambazo zimetumika na zenyewe ni faragha, ndiyo maana katika choo hiki kuna kichomea taka,”amesema Macha.
“Mwanafunzi akikosa vipindi vya masomo sababu ya hedhi hata akili yake lazima ivurugike, nakupongeza sana Flaviana kwa kusaidia kukuza taaluma za wanafunzi wa kike, sababu hawatakuwa tena wanakosa masomo sababu ya hedhi mara baada ya kuwajengea choo kizuri chenye chumba maalumu ili wajistiri hedhi na kuwa na faragha yao,”ameongeza.

Aidha, amesema mahitaji ya vyoo bora siyo tu katika maeneo ya shule, hata watu wanapaswa katika Kaya zao wawe na vyoo vizuri, na kwamba katika Mkoa wa Shinyanga ni asilimia 77 tu ya wananchi wenye vyoo bora,lakini asilimia 23 hakuna, huku akibainisha kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika masuala ya maendeleo.
Amempongeza pia Flaviana Matata kwa juhudi zake za kusaidia na serikali katika kukuza sekta ya elimu, na kwamba licha ya kujenga vyoo vya wasichana shuleni, pia amekuwa wakiwafadhili kimasomo na hata kuwapatia taulo za kike kila mwezi, huku akimuagiza pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze kuvifanyia ukarabati pia vyoo vya wavulana ili navyo viwe na hadhi.

Mjumbe wa Bodi wa Flaviana Matata Foundation Wilhemina Malima, amesema chumba maalumu cha kujistiri hedhi ni muhimu kwa wanafunzi shuleni katika kukuza taaluma zao, sababu kwa mwezi hukosa siku tano za masomo, ambapo kwa mwaka mzima hukosa siku zaidi ya 50.
Amesema ujenzi huo wamatundu ya vyoo shuleni hapo, umesaidia pia kupunguza uwiano wa tundu moja kutumiwa na wanafunzi wengi, na kwamba shule hiyo ina wanafunzi 408 wa kike, ambao sasa hivi watakuwa akitumia tundu moja wanafunzi 34 na siyo 54 kama hapo awali.

Amesema kwa upande wa wavulana wapo 588, na kwamba matundu 8 ya zamani ya wasichana watakuwa wakiyatumia, na ukijumuisha na matundu yao 8 jumla watakuwa na matundu 16, ambapo tundu moja watakuwa wakitumia wavulana 37 kutoka zamani kutumia tundu moja wanafunzi 74.
Mratibu wa mfuko wa ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT-Trust)mkoani Shinyanga Glory Mbia, ametoa wito kwamba miundombinu ya choo hicho itunzwe pamoja na kufanyiwa usafi wa mara kwa mara, ili udumu na kuwahudumia wanafunzi kwa muda mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi hiyo Flaviana Matata, amesema wamekuwa wakiunga mkono sekta ya elimu “kusuport” wanafunzi wa kike, na katika Mkoa wa Shinyanga wamekuwa na mradi wa ujenzi wa vyoo vya wasichana vyenye chumba maalumu cha kujistiri hedhi, pamoja na kuwafadhili masomo na kuwapatia taulo za kike kila mwezi.
Amesema katika shule hiyo ya Sekondari Masekelo,wamejenga choo cha wasichana chenye matundu 12 kikiwa na chumba maalumu cha kujistiri hedhi, pamoja na kichomea taka, na wanawafadhili wanafunzi 5 kimasomo, na kwamba kila mwezi hua wanawapatia wasichana 30 taulo za kike katika shule hiyo.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi mkoani Shinyanga, kwamba waachane na tabia ya kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni, bali wawaache wasome na kutimiza ndoto zao, ili kutorudisha nyuma juhudi za wadau katika kumuinua mtoto wa kike kielimu.
Meneja Miradi kutoka Taasisi ya Flaviana Matata, Lineth Masala, amesema ujenzi wa choo hicho cha wasichana shule ya Sekondari Masekelo, umezingatia pia miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Mkuu wa shule ya Sekondari Masekelo Vicent Kanyogota, amesema upatikaji wa chumba maalumu cha wanafunzi wa kike kujistiri hedhi shuleni hapo, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro, na hata kufanya vizuri kitaaluma sababu hawatakuwa wakikosa vipindi vya masomo tena.
Mkurungenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, ameipongeza Taasisi hiyo ya Flaviana kwa kuunga mkono suala la elimu, na kwamba halmashauri itatumia kiasi cha sh.milioni 6 ili kuboresha miundombinu ya choo cha wavulana.

Nao wanafunzi wa kike katika shule hiyo akiwamo Ester Jackson, ameipongeza taasisi hiyo, kwamba hawatakuwa wanakosa vipindi tena vya masomo, sababu wanachumba cha kujistili hedhi na watafanya vizuri kitaaluma.

Ujenzi wa choo hicho cha wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Masekelo Manispaa ya Shinyanga, umetekelezwa na Taasisi ya Flaviana Matata kwa ufadhili wa Diamond Do Good.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa choo cha wasichana shule ya sekondari Masekelo.
Mjumbe wa Bodi wa Flaviana Matata Foundation Wilhemina Malima, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Foundation Flaviana Matata akizungumza kwenye hafla hiyo.
Meneja Miradi kutoka Taasisi ya Flaviana Matata, Lineth Masala, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mratibu wa mfuko wa ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT-Trust)mkoani Shinyanga Glory Mbia, akizunguza kwenye hafla hiyo.
Mkurungenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa shule ya Sekondari Masekelo Vicent Kanyogota, akisoma taarifa ya shule kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizundua choo cha wasichana shule ya sekondari Masekelo ambacho kimejengwa na Taasisi ya Flaviana Matata.
Muonekano wa choo cha wasichana shule ya sekondari Masekelo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akikagua choo hicho.
Picha za pamoja zikipigwa.
Mkurugenzi wa Foundation Flaviana Matata (kulia) akiwa na Mratibu wa WFT-Trust mkoani Shinyanga Groly Mbia kwenye hafla hiyo.
Wazazi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kushoto) akisalimia na Flaviana Matata
Previous Post Next Post