Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) ameitaka timu ya Wataalam kutoka Tanzania Bara na Zanzibar inayoshiriki katika kuandaa na kukamilisha rasimu ya taarifa ya Nchi kuhakikisha taarifa zinazoandaliwa katika kuimarisha Haki za Binadamu zinajumuisha jinsia ya Kike na Kiume na kuepuka kuimarisha kundi moja pekee kwani makundi haya yanategemeana.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo Oktoba 23, 2024 katika ukumbi wa Flomi hoteli mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha kuandaa taarifa ya Nchi ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake Afrika ambayo Nchi ya Tanzania imeridhia.
Mhe. Sagini amesema kuwa yapo baadhi ya maeneo Wanaume wameacha kutimiza wajibu wao wa msingi na kuwa wategemezi kwa Wanawake kutokana na kutojengwa vizuri katika kutambua majukumu yao ya msingi.
"Upo umuhimu kama Nchi tunapokazia Haki za Binadamu, Haki za Mtoto wa Kike,Haki za Wanawake tusisahau Haki za Binadamu, Haki za Mtoto wa Kiume na Haki za Mwanaume.
Katika jamii wapo baadhi ya Wanaume wanakwepa kutekeleza majukumu yao na wanawaachia Wanawake pekee.
Tunapoimarisha Haki za mtoto wa kike tuhakikishe tunaimarisha na haki za mtoto wa kiume na twende nazo pamoja kwa maana makundi haya mawili yanategemeana.
Kama upendeleo ulifanyika kwa watoto wa kiume ilikua ni zamani sio kwa huyu anayezaliwa sasa.
Hawa wote ni watoto wetu isije kutokea tunapendelea mtoto wa kike na kupelekea wanaume wanapokuwa watu wazima kushindwa kutimiza majukumu yao kutokana na jamii inavyokuwa imejengwa kuamini."Alisema Sagini.
Naibu Waziri Sagini amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya mabadiliko chanya na ambayo yanahitaji kuripotiwa kwa kuwa mstari wa mbele kutimiza matakwa ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kwa kuwa Serikali inayozingatia Utawala Bora na Sheria katika kuwahudumia Watanzania, bila upendeleo,udini,ukabila, jinsia na bila kujali vyama vyao vya Siasa na misimamo mingine.