Na Mapuli Kitina Misalaba
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mkoani Shinyanga,
imeanza rasmi zoezi la utoaji mikopo ya asilimia kumi kwa makundi maalum,
ambayo ni wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mheshimiwa Mboni Mhita,
amefunga mafunzo ya siku mbili kwa maafisa maendeleo ya jamii, huku akiwataka
kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa ili
kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi wa asilimia 100.
Mheshimiwa Mhita ameunda kamati maalum,
inayosimamiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, kwa lengo la kuhakikisha
uwazi, uwajibikaji, na usimamizi bora wa zoezi hilo.
“Kwa
sasa hivi kuna mfumo mpya umekuja ambao ni mzuri zaidi na upo sahihi nitumia
fursa hii sasa kuwaomba muwe makini sana timu nzima kwenye hatua kuanzia ya awali kabisa kuangalia
vikundi kuvifuatilia vikundi kuona ni vikundi gani ambayo vinakadhi vigezo
lakini kikubwa zaidi ni ufuatiliaji wa marejesho”.
“Sasa
hivi katika kuweka uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa mikopo hii ofisi ya mkuu
wa Wilaya inaunda timu maalum ya kufuatilia zoezi hili ambapo namteua katibu
tawala wa Wilaya ndiyo atakuwa mwenyekiti wa hiyo timu, namteua afisa kutoka
ofisi ya DSO atakuwepo kwenye hiyo timu, nateua afisa kutoka PCCB atakuwepo
kwenye hiyo timu, mtu kutoka jeshi la polisi atakuwepo kwenye hiyo timu na
wengine kutoka taasisi tatu”.
“Kwahiyo
kwa kifupi ni kwamba ni lazima utaratibu huu uwe na uwazi, uwe na uwajibikaji
lakini usimamizi uwe ni usimamizi ambao hauleti alama ya swali nawasihi sana
tusikwamishe malengo ya Rais Samia katika zoezi hili”.amesema
Mhe. Mboni
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Msalala, Bi. Mary Nziku, amesema kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja
na milioni 87 zimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana, na watu
wenye ulemavu. Fedha hizo zimegawanywa kwa uwiano wa asilimia 40 kwa wanawake,
asilimia 40 kwa vijana, na asilimia 20 kwa watu wenye ulemavu.
"Kiasi
cha fedha kilichotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa ajili ya mikopo
ni shilingi bilioni moja, milioni 87, laki nne na elfu 64. Fedha hizi
zitatolewa kama mikopo kwa uwiano ufuatao: wanawake watapokea asilimia 40,
ambayo ni sawa na shilingi milioni 434, laki 9 na elfu 85, na senti 88; vijana
watapokea asilimia 40, sawa na shilingi milioni 434, laki 9 na elfu 85, na
senti 88; na watu wenye ulemavu watapokea asilimia 20, sawa na shilingi milioni
217, laki 4 na elfu 92, na senti 94. Jumla ya fedha hizo ni shilingi bilioni
moja, milioni 87, laki nne na elfu 64," amesema Mary.
Baadhi ya maafisa maendeleo ya jamii kutoka kata mbalimbali za Halmashauri hiyo wameahidi kusimamia zoezi hilo kwa weledi ili kuhakikisha linafanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, akitangaza
kamati maalum kwa ajili ya ufuatiliaji wa zoezi la mikopo ya asilimia kumi
katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, akiwahimiza maafisa maendeleo ya jamii kusimamia vizuri zoezi hilo la mikopo ili kuleta matokeo chanya.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, akiwasisitiza maafisa maendeleo ya jamii kuongeza umakini ili kufanikisha zoezi hilo la mikopo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Bi. Mary Nziku, akielezea namna ya utoaji wa mikopo hiyo ambapo amesema zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni 87 zimetengwa huku akiwasisitiza wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Bi. Mary Nziku, akielezea namna ya utoaji wa mikopo hiyo ambapo amesema zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni 87 zimetengwa huku akiwasisitiza wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo.