HOSPITALI YA KOLANDOTO YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA NAMNA YA KIPEKEE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Hospitali ya Kolandoto iliyopo mkoani Shinyanga imejikita katika kuimarisha huduma bora kwa wagonjwa wake.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joseph Wallance Sahan, ameeleza kwamba juma hili ni fursa muhimu kwa Hospitali ya Kolandoto kujitathmini, kuangalia maendeleo iliyofikia, na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Dkt. Sahan amesisitiza kwamba malengo makuu ya Hospitali ni kutoa huduma bora, si bora huduma, huku akibainisha kuwa changamoto kubwa inayoikabili dunia sasa ni upatikanaji wa huduma bora zaidi kuliko upungufu wa huduma.

"Tunaliadhimisha juma hili kwa kutafakari kule tulikotoka, tulipo sasa, na tunakoelekea malengo yetu ni kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata huduma bora, si bora huduma,"  

"Kwa sasa changamoto kubwa ni huduma bora, siyo tena tatizo la kukosa huduma nchi zinazoendelea, kama yetu, zinakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora," amesema Dkt. Sahan.

Kwa kuzingatia hilo, Kolandoto Hospitali imejipanga kwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wao, kuhakikisha wanapokewa kwa lugha nzuri, yenye staha na inayojali.

Dkt. Sahan ameeleza kuwa Hospitali hiyo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa tiba, madaktari bingwa, na huduma za uchunguzi kama maabara, radiolojia, pamoja na dawa za kutosha zinazokidhi mahitaji ya sasa ya magonjwa.

Miongoni mwa mafanikio ya Hospitali ya Kolandoto ni upatikanaji wa huduma za kibingwa ambazo hazikuwa zinapatikana awali katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.

Dkt. Sahan amefafanua kuwa sasa wanatoa huduma za kibingwa kwa magonjwa ya ngozi, mifupa, macho, meno, magonjwa ya akina mama, na huduma kwa magonjwa ya ndani, koo, pua, na sikio.

Katika wiki hii maalum, Kolandoto Hospitali imejipambanua kwa kuwa na dawati maalum la kusikiliza kero, ushauri, na maoni ya wateja wao, ili kuboresha zaidi huduma zao.

Pia, hospitali hiyo imeandaa zawadi kwa wateja wanaotembelea hospitali hiyo, hatua ambayo imepokelewa vizuri na wananchi wengi waliofika kupata huduma wamepongeza juhudi za Hospitali hiyo na kuomba huduma bora ziongezwe na kudumu.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika Hospitali ya Kolandoto yanatarajiwa kufikia kilele kwa hafla maalum itakayohusisha wateja wao, ambapo keki itakatwa kama ishara ya kuonyesha uhusiano mzuri kati ya watoa huduma na wateja.

Misalaba Media imezungumza na baadhi ya wananchi waliopata huduma katika Hospitali hiyo, ambao wameonyesha kuridhishwa na huduma walizopokea, huku wakitoa wito wa huduma hizi bora kuendelezwa zaidi.Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joseph Wallance Sahan, akielezea mafanikio ya Hospitali hiyo.




Previous Post Next Post