Na Elizabeth Cornely
JUKWAA la Wafanyabiashara na Huduma(JBH) wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini.
Kauli hiyo ilitolewa Katibu Mtendaji wa Jukwaa hilo, Fredy Leopold, wakati wa uzinduzi rasmri wa jukwaa hilo uliofanyika jana jijini Dar es Salama.
Alisema wafanyabiashara nchini wanatambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia hususani katika kutatua kero zote ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara hao kwa muda mrefu ikiwamo urasimu na utitiri wa kodi.
"Tunatoa shukrani zetu kwa Rais Samia na serikali yake yote kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayofanya lakini pia kwa kutambua umuhimu sekta hii na kuimarisha mazingira ya biashara, kuendelea kuimarisha miundombinu na kuinua wafanyabiashara nchini kupitia sera rafiki ambazo serikali imeweka kwa sasa.
"Tumeshuhudia ikiendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia uboreshaji miundombinu, kuweka sera za kifedha na kupunguza urasimu katika sekta hii.
"Tumeshuhudia pia ikianza mchakato wa kuunganisha mifumo, kukamilisha miradi ya reli ya kisasa, upanuzi wa Bandari na uwekezaji katika sekta ya nishati ambavvyo vyote ni kielelezo tosha cha dhamira ya serikali katika kusaidia wafanyabiashara nchini,"alisema Leopold.
Alisema wao kama wafanyabiashara hawawezi kusahau kazi hiyo kubwa hasa katika kuweka na kujenga misingi dhabiti kwao.
"Kwa kweli jitihada hizi zinaendana kabisa na malengo ya kuanzishwa kwa jukwaa hili la biashara na huduma na tunatambua jitihada za serikai yetu katika kutufungulia fursa za kibiashara Kikanda na Kimataifa,"alisema Leopold.
Alitaja baadhi ya malengo ya kuanzisha jukwaa hilo kuwa ni pamoja na kusaidia kuunganisha wafanyabiashara, masoko pamoja na fursa mbalimbali.
Pia, alisema lengo jingine ni kusogeza huduma na kuchochea biashara kimtandao, kuimarisha mazingira ya kibiashara Tanzania hasa Kariakoo kwa kutumia teknolojia.
Kuingiza bidhaa zinazozalishwa Tanzania katika masoko ya Afrika Mashariki na SADC, wakilenga kuimarisha biashara kimatafa na kukuza zaidi uchumi wa wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.
Kadhalika, alisema jukwaa hilo litasaidia kupunguza urasimu kwa kuandaa mazingira ya uwezeshaji kupitia majadiliano kati ya wafanyabiashara na taasisi za serikali na watoa huduma wengine.
Alisema Jukwaa litasadia pia katika kutoa huduma za kiufundi na uwekezaji kwa kutoa fursa za kipekee kwa wafanyabiashara kupata huduma za kitaalamu ikiwamo usimamizi wa fedha.
Mwisho.