Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametoa maagizo kwa Mawaziri wa Kilimo na TAMISEMI kushughulikia kero zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini.
Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tinde, Dk. Nchimbi amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kutatua tatizo la upatikanaji wa mbegu za mahindi kupitia mfumo wa usambazaji ambao umekuwa ukikwamisha wakulima.
Aidha, Dk. Nchimbi amemuagiza Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kuhakikisha kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, kituo cha afya kipya kijengwe katika mojawapo ya Kata za Didia na Lyabukande, kama alivyoomba Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji huduma za afya.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi amepokea jumla ya kero 73 kutoka kwa wananchi 32, ambazo alikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ili zifanyiwe kazi. Alisisitiza kuwa kero zinazohusiana na msimu wa kilimo uliopita, ikiwemo tatizo la mbegu, zitatuliwe kabla ya msimu ujao kuanza.
Katibu wa Itikadi, Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amewasihi wananchi kuendelea kuwa na imani na Rais Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa serikali yake imeleta maendeleo makubwa na kufikia kila kijiji nchini. Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na serikali ili kufanikisha miradi zaidi.
Naye Mchungaji Peter Msigwa ameeleza kuwa Tanzania ipo katika mikono salama chini ya CCM na Rais Samia, na kwamba hakuna haja ya wananchi kuamini maneno ya wapinzani wanaodai kuleta ukombozi wakati nchi tayari imeshapata ukombozi wake.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amesisitiza kuwa Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi bilioni 846 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo, huku akiendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Tinde.Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza kwenye mkutano huo.Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza kwenye mkutano huo.Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele akizungumza kwenye mkutano huo.