Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa chama cha ACT Wazalendo jimbo la Shinyanga
mjini, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa na Naibu Waziri Kivuli wa
Jinsia, Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Bi. Juster Denis amejitokeza
kujiandikisha kwenye daftari la wakazi katika kituo cha shule ya msingi
Ndembezi.
Tukio hilo linatokea kuelekea uchaguzi wa Serikali
za Mitaa ambapo Bi. Juster amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi
ili kuchagua viongozi bora.
Bi. Juster ameeleza kuwa moja ya sababu kubwa ya
kujitokeza kwake ni kuhamasisha wananchi, hususan vijana, ili waweze kushiriki
kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi.
"Nimekuja
hapa kujiandikisha lakini pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili
tupate viongozi bora. Ni muhimu vijana wajitokeze, wasiwe wa kusema tu na
hawajajiandikisha kwenye daftari la wapiga kura,"
amesema Juster.
Bi. Juster ametumia fursa hiyo kuzungumzia
changamoto zinazolikabili eneo la Ndembezi, akitolea mfano wa miundombinu duni,
ikiwemo ukosefu wa barabara licha ya kuwa eneo hilo ni sehemu ya Manispaa.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa kiongozi bora ni
njia ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa eneo hilo.
"Hii Ndembezi ni eneo la Manispaa lakini
tangu liingizwe kwenye ramani hiyo halina barabara, ni wakati sasa wa kuchagua
viongozi wanaoweza kubadilisha hali hii tunataka mabadiliko, tuchague ACT
Wazalendo ili tuweze kuvuka kutoka tulipo kwenda sehemu nyingine,"
amesema Juster
Katika mazungumzo yake, Bi. Juster amekosoa tabia ya
wanasiasa kutumia ahadi za miradi hewa kama vile ujenzi wa zahanati ambazo
hazikamiliki kwa miaka mingi kama njia ya kupata kura.
Amesema chama chake cha ACT Wazalendo kinajikita
katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi na siyo kuahidi miradi ambayo
haitekelezeki.
"Tunamsingi wa zahanati ambao umekuwa
ukitumika kuombea kura kwa miaka mingi, sisi ACT Wazalendo hatutaki hayo tunataka
mabadiliko halisi kwa wananchi," amesema Juster.
Misalaba
Media imezungumza
na baadhi ya wanawake wakazi wa mtaa wa Ndembezi ambao tayari wamejiandikisha
kwenye daftari la wakazi na kwamba wamehamasisha wanawake wenzao kujitokeza kwa
wingi na kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi.
Wamesema ni muhimu kwa wanawake kujitokeza ili
kuhakikisha wanapata viongozi wa mtaa wanaofaa ambao watazingatia maslahi ya
wananchi wote.
Uchaguzi wa serikali za mitaa ukikaribia, hamasa inaonekana kuongezeka kwa wananchi wa Shinyanga mjini, huku viongozi wa vyama vya siasa wakihimiza umuhimu wa uandikishaji wa wakazi kama hatua ya awali ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Katibu wa chama cha ACT Wazalendo jimbo la Shinyanga mjini, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa na Naibu Waziri Kivuli wa Jinsia, Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Bi. Juster Denis akijiandikisha kwenye daftari la wakazi.