Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi
Dkt. Emmanuel Nchimbi, amechukua hatua kubwa katika kutatua changamoto za
wananchi wa Kata ya Ibadakuli kwa kutoa maelekezo ya ujenzi wa Kituo cha Afya
katika eneo hilo.
Akiwa mbele ya umati wa wananchi, viongozi wa chama
na Serikali, Dkt. Nchimbi ametoa agizo rasmi kwa Waziri wa TAMISEMI, Mohammed
Mchengerwa, kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unaanza mara moja.
Balozi Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Serikali
kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha wananchi wa Ibadakuli wanapata huduma
bora za afya.
“Nichukue
nafasi hii kumuelekeza Waziri wa TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa, popote alipo,
hili ni agizo la Chama cha Mapinduzi (CCM), kuhakikisha Kituo cha Afya
Ibadakuli kinaanza kujengwa mara moja. Natambua yeye ni miongoni mwa Mawaziri
wasikivu na wachapakazi," amesema Dkt. Nchimbi,
Agizo hili linakuja kufuatia maombi yaliyotolewa na
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye ni Naibu Waziri
katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe.
Paschal Patrobas Katambi.
Katika mkutano
huo wa hadhara, Katambi ameelezea uhitaji mkubwa wa huduma za afya kwa wananchi
wa Kata ya Ibadakuli, pamoja na umuhimu wa kukarabati Hospitali ya Manispaa na
barabara ambazo zimeathiriwa vibaya na mvua za msimu.
Amesema kuwa wananchi wa Ibadakuli wamekuwa na
changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma za afya za karibu, hivyo ameiomba
Serikali kuwekeza katika ujenzi wa kituo hicho.
Aliongeza kuwa mbali na afya, eneo hilo pia
linahitaji ukarabati wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga pamoja na barabara
zilizoathiriwa na mvua.
Mbunge Katambi pia ametumia fursa hiyo kumpongeza
Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Jimbo la
Shinyanga mjini, akibainisha miradi mingi inayotekelezwa, ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa uwanja wa ndege, miundombinu ya barabara, na Hospitali.
“Rais
Samia Suluhu Hassan amewekeza sana katika jimbo letu, na tumeona maendeleo
makubwa, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege Ibadakuli, barabara, na madaraja.
Hata hivyo, tunahitaji zaidi katika sekta ya afya na miundombinu,” naomba
mfikishe salamu za shukrani kwa Rais kutokana na miradi hiyo ya maendeleo”.
“Tunatoa
shukrani za dhati kwa Rais wetu kwa fedha nyingi alizotoa kwa ajili ya
kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya, Hospitali, na
zahanati saba za kisasa,” amesema Katambi.
Mhe. Katambi
amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi zake nzuri za
kuwaletea maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi ameagiza
ushirikiano baina ya Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Ulinzi, Dkt. Stergomena
Tax, kuhakikisha mgogoro baina ya Jeshi na wananchi wa Shinyanga unatatuliwa
kwa njia ya amani.
Ameitaka
TARURA kuharakisha ukarabati wa barabara zote zilizoharibika, ili wananchi
waendelee kunufaika na miundombinu bora.
Akihitimisha hotuba yake, Katibu Mkuu Nchimbi ametoa
wito kwa wananchi wa Shinyanga kujiandikisha kwenye daftari la wakazi, ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika
Novemba 27.
Amesisitiza kuwa zoezi la kujiandikisha linaendelea
hadi Oktoba 20 na akatoa mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye tayari
amejiandikisha.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi, na Mafunzo, Ndugu
Amos Makalla, ameungana na viongozi wengine kumpongeza Mbunge Mhe. Katambi kwa
juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
Amewaambia wananchi kuwa Shinyanga ya sasa si ile ya
zamani, kwani imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na uwekezaji wa Serikali
ya awamu ya sita.
MISALABA
MEDIA imezungumza na baadhi ya wakazi wa Shinyanga Mjini
ambao wametoa pongezi kwa Mbunge wao, Mhe. Patrobas Katambi, kwa juhudi zake za
kufikisha changamoto zao kwa viongozi wa kitaifa.
Wakazi hao wamesema wanathamini kazi nzuri
anayofanya Mbunge wao na wana imani kuwa Serikali itashughulikia haraka
changamoto alizozibainisha, hususan uhitaji wa Kituo cha Afya katika Kata ya
Ibadakuli.
Aidha, wakazi hao wameeleza kuwa ujenzi wa barabara
kwa kiwango cha lami ni kipaumbele kwao, hasa barabara ya kutoka Ndala kwenda
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mwawaza ambapo wamesisitiza kuwa
barabara hiyo ni muhimu kwa usafiri wa wagonjwa na pia itaongeza ufanisi wa
huduma za afya katika Hospitali hiyo.
Wananchi hao wamesema wanatumaini kuwa hatua hizo
zitachukuliwa kwa haraka ili kuboresha huduma za jamii na kuwezesha wananchi
kupata maendeleo yanayoendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Ziara ya Dkt. Nchimbi katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga imetamatika kwa mafanikio makubwa, huku lengo kuu likiwa ni kukagua kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo mbalimbali.
TAZAMA VIDEO