Na Mapuli Kitina Misalaba
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ametoa
ombi la kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara na huduma za umeme katika Wilaya
ya Kahama wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 10, 2024 Manispaa ya
Kahama.
Akizungumza
mbele ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,
pamoja na wananchi wa Kahama, Mhe. Cherehani amegusia mafanikio ya utekelezaji
wa miradi lakini pia amesisitiza umuhimu wa marekebisho kadhaa katika huduma
zinazotolewa na taasisi za umma.
Mhe. Cherehani amebainisha kuwa moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni upungufu wa
usimamizi wa barabara katika Halmashauri ya Ushetu.
“Halmashauri ya Ushetu ilikuwa na Meneja wa
TARURA aliyekuwa anasimamia barabara zote, lakini aliondolewa na sasa
tunategemea meneja mmoja aliyepo Kahama eneo la Kahama ni kubwa sana, na hili
linatuathiri tunaomba turudishiwe meneja
wetu ili kuhakikisha barabara zinakaguliwa ipasavyo na ziko katika hali nzuri,”
amesema Chelehan.
Mhe. Cherehani pia amezungumzia changamoto ya kuwa na
mkandarasi mmoja anayesimamia miradi ya ujenzi wa barabara katika majimbo yote
matatu ya Wilaya ya Kahama - Ushetu, Msalala, na Kahama Mjini.
"Wilaya
ya Kahama ni kubwa sana, lakini tunapewa mkandarasi mmoja tu kwa majimbo yote hili
linaathiri kasi ya utekelezaji wa miradi, na wakati mwingine mkandarasi
anakosolewa kwa kutokukamilisha kazi kwa wakati, ilhali ukubwa wa eneo ni
changamoto kubwa kwake,” ameeleza Cherehani.
Ameendelea kuomba kuwa kila jimbo lipatiwe
mkandarasi wake wa ujenzi ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi zaidi
na kwamba ombi hili linaonekana kuwa la msingi, ikizingatiwa kuwa wilaya hiyo
ina jiografia kubwa na miradi mingi inahusisha maeneo ya mbali.
Kahama
Iwe Mkoa wa Ki-Tanesco
Katika hatua nyingine, Mhe. Chelehan amezungumza
kuhusu tatizo sugu la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Wilaya ya Kahama
ambapo ameomba Kahama ipandishwe hadhi kuwa Mkoa wa Ki-Tanesco ili kuhakikisha
huduma za umeme zinaboreshwa.
"Umeme unakatikakatika sana, hali hii
inawaathiri sana wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wafanyabiashara
wanapata hasara, na bei ya jenereta imepanda sana tunaomba Mkoa wa Ki-Tanesco
ili na sisi Ushetu na Msalala tuweze kupata umeme wa uhakika,”
amesema Cherehani.
Cherehani ameeleza kuwa kutokana na shughuli nyingi
za kiuchumi katika wilaya hiyo, hasa za uchimbaji madini, kuna umuhimu mkubwa
wa kuwa na usimamizi wa umeme wa karibu ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa
uhakika na endelevu.
Katibu
Mkuu CCM Apiga Simu kwa Waziri Biteko
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,
amelazimika kumpigia simu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto
Biteko, kwa lengo la kupata muafaka kuhusu ombi hilo la kuongeza Mkoa wa
Ki-Tanesco Kahama.
Katika mazungumzo ya simu, Mhe. Biteko amekiri kuwa
Wabunge wa Kahama wamewasilisha maombi hayo mara kadhaa, na serikali tayari
imelifanyia kazi suala hilo ambapo amesema kuwa utekelezaji wa mpango huo
utaanza katika mwaka wa fedha 2024/2025.
"Tulipokea maombi kutoka kwa wabunge wa Kahama,
na tumefanya uchambuzi wa kina kwenye maeneo yatakayopatiwa Mkoa wa Ki-Tanesco,
Kahama itakuwa miongoni mwa maeneo yatakayopata huduma hii kutokana na umuhimu
wake wa kiuchumi, hasa kutokana na migodi ya madini iliyopo katika eneo
hilo," ameeleza Mhe. Biteko.
Mkutano huo umehudhuriwa na mamia ya wananchi wa
Wilaya ya Kahama, ambapo Mhe. Chelehan ametumia nafasi hiyo kuelezea juhudi
zake katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Amejivunia kuwa tangu awe mbunge, amefanya mikutano
274 ya hadhara, na kwa kushirikiana na viongozi wa kata, matawi, wilaya, na
mkoa, amefanikiwa kutatua kero nyingi za wananchi.
Amewapongeza viongozi wa serikali, akiwemo Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, kwa ushirikiano mkubwa
wanaouonesha katika kuleta maendeleo Ushetu.
Baada ya mkutano huo wa hadhara, Misalaba Media
imezungumza na baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kahama, wakiwemo wananchi wa Jimbo
la Ushetu, ambao wamempongeza Mbunge wao, Mhe. Emmanuel Cherehani, kwa juhudi
zake za kusimamia maendeleo ya jimbo hilo.
Wakazi hao wameeleza kuwa changamoto alizozitaja
mbunge zinaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi, huku wakiiomba
serikali kuharakisha utatuzi wa matatizo hayo.
Wameeleza matumaini yao kwamba ombi la kuongeza Mkoa
wa Ki-Tanesco litafanikishwa, wakiamini kuwa litasaidia kupunguza matatizo ya
umeme ambayo yamekuwa yakiathiri biashara na maendeleo ya kijamii katika wilaya
hiyo.
Kwa ujumla, wananchi wa Ushetu wamepongeza jitihada
za Mhe. Chelehan, huku wakiendelea kuiomba serikali kushughulikia changamoto
zilizopo kwa haraka ili kuboresha maisha yao na kuimarisha uchumi wa wilaya,
mkoa, na taifa kwa ujumla.
Mkutano huu umetoa picha ya juhudi kubwa
zinazofanywa na Mbunge wa Ushetu kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma
bora na miundombinu iliyoboreshwa pia umetoa matumaini kwamba ombi la Kahama
kuwa Mkoa wa Ki-Tanesco litafanikishwa na serikali ndani ya muda mfupi.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Chelehan akielezea changamoto za wananchi katika mkutano wa hadhara Wilaya ya Kahama.