Na Sheila Katikula, Dodoma
Diwani wa Kata ya Mondo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba iliyopo mkoani Dodoma Mheshimiwa ,Said Sambala amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kata hiyo fedha nyingi za miradi ya maendeleo hususan katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii katika kata hiyo.
Hayo ameyasema juzi kwenye mahafali ya mahafali ya 27 ya Shule ya Sekondari ya Mondo iliyoko Kata ya Mondo Wilaya ya Chemba mkoa wa mkoni Dodoma.
Mheshimiwa Sambala amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Sh Bilioni Moja na Milioni Miatatu kwenye Kata yetu ya Mondo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo elimu na vile vile ametuongezea Sh Milioni Mia Moja kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Waida tunajukumu la kuunga mkono juhudi hizi za Rais.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na sekta ya afya, elimu, maji hivyo amewataka wananchi wa Kata hiyo kuunga mkono juhudi za Rais kwa kutunza miradi hiyo ili waweze kutumia kwa muda mrefu.
Hata hivyo amewataka wazazi kuwapatia watoto wao mahitaji ya msingi ili waweze kwenda shule kwa wakati sanjali na kuwapatia chakula.
Hata hivyo katika kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo ya utoro Mheshimiwa Sambala amemshauri Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Thomas Chorray kuitisha kikao cha haraka ili waweze kujadili changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi ili wanafunzi hao waweze kutimiza ndoto zao za baadaye.
"Nadhani kuna haja ya Bodi ya Shule tukutane haraka kuzipatia ufumbuzi changamoto za shule hii ikiwemo changamoto sugu ya utoro.
Sambala amesema utoro tafsiri yake ni moja tu kwamba mahala fulani jamii yetu hatuko sawa kauli hii ameitoa kufuatia takwimu za wahitimu wa mwaka huu kuonesha karibu nusu ya wanafunzi 103 kati yao wavulana 36 na wasichana 67 wameshindwa kuhitimu kwa sababu ya utoro ikilinganishwa na wanafunzi 112 kati yao wavulana 54 na wasichana 68 waliohitimu leo.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Sambala amewataka wahitimu wa miaka ya nyuma waliomaliza kwenye shile hiyo kuungana katika kutatua changamoto za shule hiyo.
"Mimi ni mmoja wa wahitimu wa shule hii pamoja na wenzangu Mkuu wa Shule Msaidizi na Mjumbe mmoja wa Bodi ya Shule ninawaomba kutumia fursa hii watu wote tuliosoma hapa kuunganisha nguvu zetu na kuanzisha utaratibu maalumu wa kurudisha fadhila kwa shule yetu kufanya hivi
tutapunguza changamoto zinazoikabili shule yetu"
Vile vile Mheshimiwa Sambala ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wa Kata hiyo kwa ujumla kujitokeza kwenye zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili kupata sifa ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
"Ninawaomba wananchi kwa ujumla tuhimizane kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili tupate sifa ya kushiriki uchaguzi unataraji kufanyika Novemba 27 mwaka huu",amesema Mheshimiwa Sambala.
Mahafali hayo yamekutanisha watu mbalimbali akiwemo Profesa Fadhil Hamza Mgumia kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo Profesa Hozen Mayaya.