Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkurugenzi wa THE BSL INVESTMENT COMPANY LIMITED na
THE TRUE LIFE FOUNDATION, Peter Frank maarufu kama Mr. Black, leo amekabidhi
msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni tatu na laki
mbili (Tsh 3,200,000) kwa shule na vikundi vilivyopo Manispaa ya Shinyanga.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika mjini
Shinyanga, huku ikihudhuriwa na viongozi wa elimu, walimu, na wanajamii wa
Shinyanga.
Msaada huo umejumuisha mabati, mifuko ya Saruji,
kompyuta, vifaa vya michezo, pamoja na viti kwa ajili ya vikundi vya kijamii
ambapo Shule zilizopokea msaada ni pamoja na Shule za Msingi Ushirika, Uhuru, Bugoyi
B, Mapinduzi A, na Town vilevile, Shule za Msingi Mwenge na Kambarage, pamoja
na timu ya vijana ya Kapina FC, wamepokea jezi za michezo.
Pia, ametoa viti 20 kwa vikundi vya Wakatoliki na
Wazazi vilivyopo kata ya Kizumbi kama sehemu ya kuimarisha uchumi wa vikundi
hivyo kwa kupitia kukodisha viti hivyo. "Nimewakabidhi viti ambavyo walivihitaji kwa ajili ya kukodisha ili
wainuke kiuchumi,".
“Leo Shinyanga tunatoa zawadi ya shukrani kwenu kwa sababu mmekuwa mkitubeba katika shughuli zenu, mmekuwa mkitubeba katika makanisa yenu, na mmekuwa mkitubeba katika vikundi vyenu ama ofisi zenu mbalimbali leo tumekabidhi vifaa vyenye thamani ya milioni tatu na laki mbili kama shukrani yetu ya dhati kwa ofisi ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo, na huu ni mwanzo tu, tutakuja tena na awamu ya pili."amesema Mr. Black
Mr. Black ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya
sadaka na shukrani kwa jamii ya Shinyanga, akisisitiza kuwa yeye ni mdau namba
moja wa maendeleo katika sekta za elimu, jamii, na uchumi nchini Tanzania.
"Nafanya
haya yote kwa sababu ni sadaka iliyotukufu kutoka ndani ya moyo wangu na ni
shukrani kwa watu wanaonisaidia katika shughuli zangu, Manufaa ya kwanza
kuyaona mimi ni kuona nchi yangu inapata maendeleo na amani."amesema Mr.
Black
"Rai
yangu kwenu, tafsiri za Shinyanga ni nyingi, lakini viongozi ninaowatambua ni
wachache wa kwanza ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wa pili ni Mbunge wangu, Paschal Patrobas Katambi, na wa tatu ni
Diwani wa Kata ya Kizumbi, Reuben Kitinya wengine waliopo katika nafasi zao pia
nawathamini, lakini naomba tafsiri potovu zisiwepo huu msaada ni wa upendo, si
wa kisiasa, na muda wa Mungu utakapofika, jina langu litakamilika."amesema
Mr. Black
Mr. Black ameeleza historia yake yenye kutoa machozi
na jinsi alivyolelewa ndani ya chama cha CCM baada ya wazazi wake kufariki akiwa
mtoto mdogo ambapo amesema kuwa msaada anaoutoa unamtoa faraja na matumaini kwa
jamii ambayo imekuwa ikimsaidia, huku akiahidi kuendelea kuwekeza katika
maendeleo ya jamii.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, mwakilishi wa Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, Lucas
Mzungu ametoa pongezi kwa Mr. Black na kampuni ya THE BSL INVESTMENT COMPANY
kwa juhudi za kurudisha fadhila kwa jamii.
"Naishukuru
kampuni ya THE BSL kupitia mkurugenzi wake Mr. Black kwa hiki wanachokifanya
cha kurudisha fadhila kwa jamii iliyowalea ni tukio la kufurahisha na lenye
baraka. Mungu awabariki," amesema Mzungu.
Aidha Mzungu amewahimiza wale waliopokea msaada huo
kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuendelea
kumpa matumaini Mr. Black na wafadhili wengine.
Walimu kutoka baadhi ya shule zilizopokea msaada huo
wamemshukuru Mr. Black kwa msaada huo, wakisema kwamba utaenda kutatua
changamoto zilizokuwepo katika shule zao huku wakimuomba aendelee na moyo huo
wa majitolea kwa jamii ya Shinyanga.