MSEMAJI MKUU WA SERIKALI: KUPAA KWA UCHUMI WA TANZANIA KUTAONGEZA UWEKEZAJI NCHINI


Na Mwandishi wetu, Dodoma.
Imeelezwa kuwa ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), inayoonesha kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia sita mwaka 2025, itasaidia kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuongeza kiwango cha uwekezaji na hivyo kuongeza ajira na kupunguza umasikini.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 24, 2024, Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba, amesema kuwa taarifa hiyo ya IMF inatoa taswira chanya kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kujenga imani kubwa wadau mbalimbali kuwekeza hapa nchni.

“Tarehe 22 Oktoba 2024, Shirika la Fedha Duniani (IMF) wamezindua ripoti ya hali ya uchumi duniani (World Economic Outlook) kwa mwaka 2024 na Serikali inajivunia taarifa njema kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia sita kwa mwaka 2025 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2024. Kutokana na ukuaji wa pato la taifa (GDP) Tanzania inakuwa kati ya nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na kwa ustahimilivu, ameeleza Bw. Makoba.

Amesema kuwa kutokana na kukua huko kwa uchumi , Tanzania inatarajia kupokea ongezeko kubwa la uwekezaji, kukua kwa sekta zingine za kiuchumi kama viwanda na kilimo, na kuchangia katika kuondoa umasikini wa mtu mmoja mmoja. 

“Ni dhima ya Serikali ya awamu ya sita kuendelea kuweka mazingira rafiki zaidi ili kuwezesha uchumi wetu kukua zaidi kiushindani duniani, amesisitiza Msemaji Mkuu wa Serikali.

Akielezea kuhusu maendeleo ya zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa baada ya zoezi la uandikishaji kukamilika, kinachoendelea sasa ni wananchi waliojiandikisha kukagua orodha katika daftari walilojiandikisha ili kama kuna changamoto zozote basi waombe kurekebisha.

Amesema changamoto hizo zinaweza kuwa kurekebisha majina kama yalikosewa, kufuta jina kama aliyejiorodhesha amefariki au hakuwa na sifa na kuongeza kuwa ukaguzi huo ulioanza tangu tarehe 21 Oktoba unaendelea mpaka tarehe 27 Oktoba, 2024 na kwamba wananchi wote waliojiandikisha ni muhimu wakajitokeza kuhakiki orodha hiyo.

Amesema muwa kama kuna Mtanzania mwenye malalamiko au hoja kuhusu zoezi zima kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa basi ni vema akawasilisha hoja zake kwa mujibu wa kanuni ya 11 (4) na (5) ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa za mwaka 2024, Tangazo la Serikali Na. 571, 572, 573 na 574 la tarehe 12 Julai, 2024 na Kanuni ya 10 (4) na (5) ya Kanuni za Uchaguzi za Serikali za Mitaa za mwaka 2024. 

Katika hatua nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali, ameviasa vyombo vya habari kuzingatia sheria, maadili na weledi katika uandishi wa habari na kwamba Saerikali ya awamu ya sita inaendelea kuchua hatua na kuweka mikakati kuhakikisha inaimarisha uhuru wa vyombo vya habari.

Amesisitiza kuwa pamoja na kwamba Serikali inaimarisha uhuru wa vyombo vya habari lakini ni vema vyombo hivyo vikatambua kuwa hakuna uhuru usiokuwa na wajibu na hivyo kila chombo cha habari kikafanya kazi kwa kuzingatia weledi na uzalendo kwa nchi.

Serikali inatambua kuwa kwa sasa dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya taarifa za vyombo vya habari kama silaha dhidi ya watu, makundi au serikali kwa maana ya weaponization of information.

 Mtakumbuka, kuna nchi ziliingia kwenye changamoto na matatizo mengi ikiwemo vita kwa sababu ya uholela, uchochezi na hulka mbaya ambayo zilichochewa na vyombo vya habari, hivyo ni kiu ya Serikali kuona tunakuwa na vyombo vya habari vyenye kufanya kazi kwa waledi na kizalendo kwa maendeleo ya wananchi wote, amesisitiza Bw. Thobias Makoba.

Mwisho 



Previous Post Next Post