Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mhe. John Siagi, amejiandikisha rasmi katika daftari
la wakazi katika zoezi linaloendelea la kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya
uchaguzi wa serikali za mitaa Mwaka huu 2024.
Zoezi hilo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya
uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Mhe. Siagi
amesema kuwa ni furaha kwake kushiriki katika zoezi hilo, ambalo linahusisha
wananchi wa Shinyanga na maeneo mengine nchini.
"Siku
ya leo na mimi nimejitokeza kujiandikisha katika zoezi ambalo linaendelea la
kupata takwimu za wakazi katika daftari la wapiga kura, hususani kwa ajili ya
uchaguzi wa serikali za mitaa," amesema Siagi.
Mhe. Siagi ameelezea kuwa alikosa fursa ya kushiriki
kwenye uzinduzi wa zoezi hili kutokana na kuwa na majukumu ya ziara ya Katibu
Mkuu wa CCM, lakini amepata nafasi leo kuungana na familia yake katika zoezi
hilo muhimu.
"Itakumbukwa
wakati wa uzinduzi wa zoezi hili, sisi baadhi ya viongozi tulikuwa na ugeni wa
ziara ya Katibu Mkuu wetu wa Chama cha Mapinduzi, hivyo basi leo nimepata fursa
kuja kuungana na wenzangu kufanikisha zoezi hili mimi pamoja na familia yangu,"
ameongeza Siagi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa zoezi hilo, Mhe. Siagi ametoa
wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili
kuhakikisha wanajiandikisha kwa wakati.
“Nitoe
wito kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi, wananchi wenye mapenzi mema na chama
chetu, lakini pia wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla, tujitokeze kwa
wingi kwa sababu tumepewa siku kumi za kutosha. Zoezi hili linakwenda mpaka
tarehe 20, kwa hiyo tujitokeze kwa wingi tutumie fursa hii ili tuweze
kuwachagua viongozi wetu,” amesema Mhe. Siagi.
Wakati huo huo, Mhe. Siagi amewahimiza viongozi wa chama kuendelea
kuhamasishana na kutoa elimu kwa wanachama na wananchi kuhusu umuhimu wa
kujiandikisha.
"Rai
yangu kwa viongozi wenzangu na wanachama wenzangu ni tuendelee kuhamasishana,
tupeane elimu ili kufanikisha zoezi la uandikishaji katika daftari la
wakazi,"
Uandikishaji huu unafanyika kwa siku kumi hadi
Oktoba 20, 2024, na utatumika kwa wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za
mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Novemba mwaka huu.
Zoezi hilo linaangaliwa kama moja ya hatua muhimu
katika kuimarisha demokrasia na kuhakikisha ushiriki wa wananchi kwenye uongozi
wa mitaa.