Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa taasisi ya Nasimama na Mama Mkoa wa
Shinyanga, CDE. Oscar Kaijage Kaindoa, amewakumbusha wana-CCM
na Watanzania kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kujitokeza kujiandikisha kwenye
daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa,
vijiji, na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza Misalaba Media baada ya kujiandikisha
kwenye daftari la wakazi, Kaindoa amesema kwamba uchaguzi huu ni fursa muhimu
kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa kuwapata viongozi
watakaoleta maendeleo ya karibu zaidi kwenye jamii zao.
"Ni jukumu la kila mwananchi aliye na sifa
kujiandikisha na kutumia haki yake ya kupiga kura ili kupata viongozi bora
wanaoweza kusimamia masuala muhimu ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo katika
maeneo yao," amesema Kaindoa.
Pia amewasisitiza vijana, wanawake, na makundi
mengine yaliyoko pembezoni kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili sauti zao
ziweze kusikika kupitia sanduku la kura. Ameeleza kuwa kujiandikisha ni hatua
ya kwanza kuelekea kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
Uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura umeanza
hivi karibuni, na Kaindoa ameongeza kuwa muda wa kufanya hivyo ni mchache,
hivyo akawataka wananchi wasisubiri dakika za mwisho.
Kaindoa amehitimisha kwa kusema, "Mabadiliko
tunayoyataka yanatokana na uwajibikaji wetu kama wananchi, na hatua ya kwanza
ni kujiandikisha ili tupate fursa ya kuchagua viongozi wanaotufaa."
Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakuwa hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hivyo jitihada za kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu zinaendelea kufanywa na viongozi wa taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Nasimama na Mama.