Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula, ametembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo (SITE) yanayoendelea katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mlimani City.
Akiwa katika banda hilo mapema hivi leo, Kitandula aliipongeza TFS kwa jitihada zake za kutangaza utalii ikolojia, utamaduni, na urithi wa misitu nchini. Pia aliishauri TFS kuongeza nguvu zaidi katika kukuza utalii wakati wa misimu ya sikukuu, akieleza kuwa Watanzania wanapendelea kutumia kipindi hicho kwa mapumziko na burudani, maarufu kama “bata.”
“Sisi Watanzania tunapenda bata, lakini bado hatujatumia mapori yetu kikamilifu katika misimu ya sikukuu. Ni muhimu tuyatangaze zaidi ili Watanzania waweze kufurahia bata huku wakiwa kwenye mandhari ya misitu yetu,” alisema Naibu Waziri Kitandula baada ya kupokea maelezo mafupi kutoka kwa Mhifadhi wa TFS, Karimu Solyambingu, kuhusu shughuli za utalii ikolojia zinazotolewa na Wakala.
Afisa Utalii Mkuu TFS, Josephy Sendwa anasema misitu ni miongoni mwa maeneo muhimu na ya utalii yanayokuwa kwa kasi Tanzania na duniani kwa ujumla. Huu ndiyo utalii daraja la kwanza katika viwango vya Shirika la Utalii Duniani (WTO).
Anaongeza kuwa kwa sasa Wakala unaendeleza shughuli za utalii katika maeneo 33 yenye vivutio vya utalii vinavyotumika kwa ajili ya utalii wa ikolojia, utafiti, burudani za kutembea, kuendesha baiskeli na mapumziko ambayo ni; Hifadhi ya Misitu ya Mazingira Asilia 18, Misitu ya hifadhi ya Asili mitatu, mashamba ya miti sita na vituo vya malikale sita
"Katika juhudi za kuendeleza na kukuza utalii wa misitu, TFS kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeendelea kutangaza vivutio vya utalii wa ikolojia na Nyuki, na utamaduni kupitia maonesho na misafara ya ndani na nje ya nchi. Maonesho ya SITE 2024 yanatarajiwa kufungua fursa mpya kwa TFS na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya utalii," anasema.
Maonesho ya SITE, yanatarajiwa kufikia kikomo kesho Oktoba 13, 2024.