SMAUJATA WATOA ELIMU DHIDI YA UKATILI SHULE YA MSINGI BALINA (BALINA ENGLISH MEDIUM) MANISPAA YA SHINYANGA


Mkuu wa Idara ya Vijana,Hamasa na Mahusiano wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kitaifa na kimataifa Bwn. Ramadhani Mohamed  Shabani amewataka viongozi wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Shinyanga kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea bila kukwamishwa na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ili kuunga kampeni kampeni ya Kitaifa ya kuhamasisha wananchi kupinga ukatili katika Jamii.

Akizungumza wakati wa kikao cha ndani kilichofanyika katika Ofisi za SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga Bwn. Ramadhan Mohamed Shaban amewasisitiza viongozi wote kufanya kazi kwa kujituma na  ushirikiano ili kuisaidia jamii kuelewa madhara yatokanayo na ukatili na njia bora za kupinga ukatili. 

‘‘ Kazi tuliyonayo ni kazi kubwa sana tusifikilie kuwa ni nyepesi unaweza kuchukiwa na watu kwa sababu ya kutetea haki za mtu mwingine tusichoke bali tunatakiwa kuwa na dhamira ya  kufanya kazi kwa ushirikiano,upendo,kujituma,uvumilivu na kuheshimiana ili tufanikishe dhamira yetu ya kuisaidia jamii kuelewa madhara yanayotokana na ukatili na jinsi ya kushiriki kupinga kila aina ya ukatili unaojitokeza’’

Baada ya kikao cha ndani viongozi hao wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Vijana,Hamasa na Mahusiano wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kitaifa na kimataifa Bwn. Ramadhani Mohamed  Shabani wametembelea katika shule ya msingi Balina (Balina English Medium) ili kutoa Elimu ya kupinga ukatili.

Akitoa Elimu hiyo kwa wanafunzi Katibu wa SMAUJATA kanda ya Ziwa Bwn. Daniel Kapaya amewasisitiza  wanafunzi wote kutoa taarifa za ukatili kwa wakati sahihi pamoja na kupunguza mazoea hatalishi yanayoweza kuchochea ukatili.

‘‘ Mtu yoyote ambaye atakufanyia ukatili au ukiona viashiria vya kufanyiwa ukatili kwako au kwa mtu mwingine hakikisha unatoa taarifa mapema kwa viongozi aidha hapa shuleni au nyumbani kwa wazazi wako usiogope lakini pia mpunguze mazoea yaliyopitiliza kwa kila mtu mfano kuna babu zetu wale wanaokuita mke wangu waambie SMAUJATA wanakemea hilo huo ni ukatili’’

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga Bwn. Mwarabu  Hakim Mhimbili amewasisitiza wanafunzi kufahamu na kuzielewa aina nne za ukatili uliopo katika jamii ili waweze kuepukana nazo.

‘‘Ni lazima tuzifahamiu aina zote nne za ukatili ili tuanze kupambana nazo kwanza kabisa kunaukatili wa kingono,ukatili wa kisaikolojia,ukatili wa kiuchumi na ukatili wa kimwili hizi zote ni aina za ukatili usimfanyie mwenzako na wewe usikubali kufanyiwa ukifanyiwa toa taarifa kwa waalimu au kwa wazazi wako na mzingatie kusoma kwa bidii ili mtimize ndoto zenu’’

Kwa upande wake Polisi Kata kutoka kata ya Ndala Afande Wila amewataka watoto wote kujiepusha na vishawishi vya kudanganyiwa vitu mbalimbali ikiwemo fedha.

‘‘Watoto mjiepushe na vishawishi kuna watu mnaishi nao katika jamii ni watu wazima wanawadanganyia pipi,hela, juice,jojo na maandazi mjiepushe na hivyo vyote msikubali waambieni huo ni ukatili’’

Akitoa neno la shukrani baada ya Elimu hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Balina Rameck William ameuomba uongozi wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga kuendelea kuwatembelea wanafunzi hao ili waendelee kujifunza zaidi namna ya kupinga ukatili na kuwakumbusha wazazi na walezi kutokuwa sehemu ya kufanya ukatili.

‘‘Niwashukuru viongozi wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga na niwaombe sana muendelee kuja kuwaelimisha hawa watoto ili watambue madhara yatokanayo na ukatili na namna ya kuepukana navyo lakini pia wazazi na walezi wenzangu sisi wenyewe tusiwe sehemu ya matukio mbalimbali ya ukatili’’

Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Shule ya msingi Balina iliyopo Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa SMAUJATA, Walimu na wanafunzi wa shule ya Msingi Balina.






























































































 



Previous Post Next Post