Leo imekuwa siku maalum kwa waumini
wa Kigango cha Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, ambao wamekusanyika kwa ajili ya
kusherehekea somo wa kigango chao.
Tukio hilo muhimu limejumuisha
Harambee ndogo yenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kupaka rangi kigango
hicho na kumalizia baadhi ya vipengele vya ujenzi wa eneo hilo la ibada, ili
kukifanya kionekane na kustawi zaidi kwa utumishi wa Mungu.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na
viongozi mbalimbali pamoja na waumini kutoka sehemu mbalimbali, huku Parokia ya
Buhangija ikiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Ndugu Charles Kidola Njange,
ambaye ametoa mchango wa shilingi milioni moja
(1,000,000) kwa niaba ya parokia ya Buhangija.
Akiongea kwa niaba ya Parokia ya
Buhangija, Njange ametoa wito kwa waumini na wakazi wa Ibadakuli kuendelea
kushikamana na kusaidia kugharamia maendeleo ya kigango hicho ili kiweze
kufikia hadhi ya kuwa parokia kamili siku za usoni.
Pia, katika sherehe hiyo,
ilikumbukwa kuwa Kigango hiki kipo ndani ya Utemi wa Busiya, jambo lililozidisha
umuhimu wa tukio hilo ambapo Mtemi wa Busiya uliwakilishwa na Bwana Nicholaus
Luhende, ambaye ametoa ahadi ya mchango wa shilingi milioni tatu (3,000,000) kwa niaba
ya familia ya Mtemi Edward Makwaia ili kusaidia gharama za kupaka rangi kigango
hicho.
Bwana Luhende amebainisha kuwa
Mtemi Edward ni sehemu ya jamii ya Kigango cha Ibadakuli, na kwa namna hiyo,
familia ya Mtemi itaendelea kushirikiana na kigango katika mipango yote ya
maendeleo kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu zamani.
Wakili Paroko wa Buhangija, Padri Sosthenes Ntemi, ametumia fursa hiyo kuwasihi waumini wa Ibadakuli kutumia michango
iliyopatikana kwa uangalifu na kwa uwazi, ili kuendelea kuvutia michango zaidi
na kuhamasisha watu kushiriki katika miradi ya maendeleo.
"Tunatamani
kuona Kigango cha Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kinakuwa kielelezo cha ushirikiano
na upendo wa jamii hii, hivyo tutumie michango hii kwa hekima ili kufikia
malengo tuliyojiwekea," amesema Wakili Padri Ntemi.
Katika Harambee hiyo, jumla ya
shilingi milioni 6,425,800 zimepatikana kupitia michango ya taslimu, ahadi, na
benki na kwamba kati ya fedha hizi, shilingi 2,600,800 zilipatikana taslimu,
shilingi 3,625,000 kupitia ahadi mbalimbali, na shilingi 200,000 zilitolewa kwa
njia ya benki.
Michango
iliyopatikana:
- Taslimu: 2,600,800/=
- Ahadi: 3,625,000/=
- Benki: 200,000/=
Jumla: 6,425,800/=
Wakili Padri Ntemi amewahimiza waumini na
wadau wengine wanaopenda kuchangia jitihada hizi kufika mbele na kutoa michango
yao, akisisitiza kuwa michango yote itasaidia kutimiza ndoto ya kuwa na Parokia
ya Ibadakuli siku za usoni.
Hafla hiyo imeleta mshikamano wa kijamii, na waumini wameahidi kuendelea kushiriki kwa ukarimu katika kukiendeleza kigango chao ambapo viongozi wa dini na jamii wanatarajia michango zaidi kutoka kwa wale ambao hawakuweza kuhudhuria hafla hiyo, ili kufanikisha lengo la kufanya kigango hiki kuwa na sura mpya inayovutia.
Mwonekano wa kanisa la mtakatifu Yohane Paulo wa pili Ibadakuli.