RAIS WA ZANZIBAR, DKT. MWINYI AONGOZA HAFLA MAALUM YA SHUKRANI YA "UZAZI NI MAISHA" KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO



 
04 Oktoba 2024, Zanzibar: Katika jitihada za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameongoza hafla maalum ya Shukrani ya "Uzazi Ni Maisha"Oktoba, 04  2024 Ikulu Mjini Zanzibar. 

Tukio hilo, ambalo limefanyika likiwakilisha awamu ya tatu ya program ya Uzazi Ni Maisha chini ya kauli mbiu “Changia Vifaa Tiba kwa Uzazi Salama”, liliandaliwa na Shirika la Amref Health Africa -Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Absa Tanzania na Wizara ya Afya ya Zanzibar.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wageni mashuhuri zaidi ya 300 kutoka sekta tofauti wakiwemo viongozi wa makampuni mbalimbali, mashirika, wanadiplomasia, taasisi za serikali, washirika wa maendeleo, jumuiya za wanadiaspora na wawakilishi wa vyombo vya habari. Hafla hiyo mbali na kusherehekea mafanikio na mchango wa wadau wote tangu kuzinduliwa kwa program ya Uzazi ni Maisha mwaka 2021, pia ililenga kukusanya fedha za ziada kusaidia azma ya serikali ya kumarisha uzazi salama.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi aliipongeza Amref Health Africa -Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Absa Tanzania na Wizara ya Afya ya Zanzibar katika kuendesha program hiyo, huku akitoa shukrani za dhati kwa wafadhili na wadau wote kwa kujitolea kwao. 

Alisisitiza umuhimu wa mchango huo katika kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga, na kutoa wito wa kuendelea kuungwa mkono na makampuni mbalimbali na mashirika ili kufanikisha azma hiyo.
“Leo tunasherehekea hatua muhimu katika juhudi zetu za kupunguza vifo vya mama na mtoto,” Rais Mwinyi alisema. 

“Tunafanya kazi kuelekea malengo makubwa: kupunguza vifo vya mama hadi chini ya 70 kwa kila vifo 100,000 vya uzazi hai, vifo vya watoto wachanga hadi 12 kwa kila vifo 1,000 vya uzazi hai, na vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi 25 kwa kila vifo 1,000 vya uzazi hai ifikapo mwaka 2030. Licha ya maendeleo, bado tunakutana na changamoto, hasa katika kupata rasilimali zakutosha kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba. Nahimiza wadau na washirika zaidi kujiunga nasi ili kufikia malengo haya.”

Mkurugenzi Mkazi wa Amref Health Africa-Tanzania Dkt. Florence Temu, alitoa shukrani kwa washirika wote ambao wamechangia kufanikisha program ya Uzazi ni Maisha. Alisisitiza dhamira ya Amref kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar katika kuboresha uzazi salama na afya ya mama na mtoto, sambamba na kupunguza vifo vya mama na mtoto katika vituo vya afya vya Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Amref Health Africa – Tanzania, Anthony Chamungwana, alisema  Amref Tanzania itaendelea kuwa mshirika thabiti katika ajenda ya huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage). “Kama ilivyobainishwa katika mpango mkakati wa Amref Tanzania wa  mwaka 2023 hadi 2030. Mkakati elekezi unazingatia huduma za afya kwa wote, mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika sekta ya afya, usalama wa afya na matumizi ya taarifa na teknolojia katika utekelezaji wa afua zetu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi S.Laiser, alisisitiza juu ya  dhamira ya benki hiyo katika kuboresha huduma za jamii. "Benki ya Absa Tanzania inajivunia kuunga mkono program ya Uzazi Ni Maisha kwa kuwa tunaamini itasaidia kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto hapa Zanzibar. Mchango wetu wa TZS 70,000,000 unaakisi kujitolea kwetu katika kuimarisha mustakabali wa Tanzania na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini."

Hadi sasa program hii ya Uzazi Ni Maisha imeweza kukusanya ahadi za jumla ya kiasi cha TZS 989,831,145 kati ya ahadi hizi imekwishapokea kiasi cha shilingi TZS 740,457,422 ambazo zimewezesha upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vya afya 28. kuhakikisha usalama na ustawi wa akina mama na watoto wachanga. Program hii imejiwekea lengo la kukusanya angalau shilingi bilioni moja, michango na ahadi mbalimbali za kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba.

Program hii itaendelea kuwa wazi kwa mwaka mmoja (mpaka 2025) ikishirikisha wadau na watu mbalimbali hadi lengo litakapofikiwa. Michango inaweza kutolewa kupitia namba ya Vodacom Lipa 5529421, Tigo 6633523 au kupitia tovuti ya wogging.amref.org.

Shukrani maalumu kutoka kwa mdhamini mkuu, Benki ya Absa Tanzania; M & D Chemical & Surgical Ltd, Tanzania Ports Authority, NBC Bank, NMB Bank, ITV/ Radio One, EATV/Radio, Swahili Sweatshop, Dalberg Tanzania, Siemens Healthcare LLC, na kila mmoja aliyewezesha Programu ya Uzazi ni Maisha) kuanzia (2022-2024) kufanikiwa.   

Previous Post Next Post