Ticker

6/recent/ticker-posts

RC MARA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA UANDIKISHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA BUTIAMA



Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi leo amefanya ziara katika Wilaya ya Butiama kufuatilia maendeleo ya uandikishaji katika daftari la mkazi kwa ajili ya  maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mtaa na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuweza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Akizungumza na wananchi katika vituo hivyo, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha pia washiriki katika kugombea nafasi mbalimbali zinazoshindaniwa katika uchaguzi huo. 
“Tuitumie fursa hii ya kikatiba vizuri ili kuwachagua viongozi wanaofaa ili waweze kusimamia miradi ya maendeleo na kushughulikia kero zetu katika maeneo yetu” amesema Mhe. Mtambi. 

Mhe. Mtambi ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wa Wilaya ya Butiama kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuongeza kuwa kwa mwitikio uliopo anamatumaini kuwa Wilaya hiyo itafanya vizuri sana katika zoezi la uandikishaji. 
Mhe. Mtambi pia amewataka wasimamizi wa uchaguzi kusimamia sheria, kanuni na taratibu lakini kama kuna changamoto zinazojitokeza kuhusiana na uchaguzi wazishughulikie mara moja ili kuondoa sintofahamu wakati huu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Kwa upande wake, Bwana Nassoro Swaibu mkazi wa Kitongoji chaKitanga, Kijiji cha Butiama amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kukitembelea kitongoji hicho kwa ajili ya kuwahamasisha kuwachagua viongozi. 
Bwana Swaibu amesema wananchi wengi wamehamasika na wanategemea kushiriki katika uchaguzi kutokana na hamasa iliyopo na ushirikiano baina ya viongozi katika Wilaya ya Butiama. 

Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Butiama Bwana Gosbert Bernard amesema jimbo hilo linategemea kuandikisha wapiga kura 183,855 na hadi tarehe 14 Oktoba, 2024 tayari watu waliojiandikisha wamefikia 53,048 ambao ni sawa na asilimia 38.8. 

Bwana Bernard amesema katika Jimbo la Butiama, mawakala wa vyama viwili vya siasa wameapishwa kwa ajili ya kusimamia uandikishaji ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hata hivyo wanaosimamia zoezi kwenye vituo mpaka sasa ni mawakala wa CCM pekee. 

Bwana Benard amesema mpaka sasa jimbo hilo halijapokea changamoto au malalamiko yoyote kutoka kwa wadau wa  uchaguzi au wananchi wa Wilaya ya Butiama na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zozote kwa kadiri zitakavyojitokeza. 

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amefanya kikao cha ndani na viongozi na maafisa wanaohusika na usimamizi wa zoezi la uchaguzi kabla ya kuvitembelea vituo vya uchaguzi na kuzungumza na wasimamizi wa vituo na wananchi waliokuwepo kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura. 
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Butiama, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama. 

Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa limeanza tarehe 11 Oktoba, 2024 na linatarajiwa kukamilika tarehe 20 Oktoba, 2024 na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika tatere 27 Novemba, 2024.













Post a Comment

0 Comments