SERIKALI YASAKA UBIA PPP KWENYE MIRADI YA KUSAFIRISHA UMEME

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali ya Tanzania imeanza mazungumzo na kampuni mbili za kigeni zenye nia ya kuwekeza jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.2 (Shilingi trilioni 3.2) kwenye miradi ya kusafirisha umeme kupitia ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

Kampuni hizo tayari zimeshaanza mazungumzo na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi (PPP Centre) kuhusu uwekezaji huo.

Iwapo watafanikiwa, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwenye historia ya nchi kutokea uwekezaji mkubwa wa njia za kusafirisha umeme kupitia ubia PPP.


Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha PPP, Bw. David Kafulila, amesema kuwa Serikali kwa sasa inajifunza kutoka kwa nchi za Latin America na Asia zenye uzoefu mkubwa wa ushirikiano wa sekta za umma na binafsi kwenye ujenzi wa miundombinu ya umeme.


Amezitaja nchi hizo kuwa ni India, Peru, Chile, Brazil na Philippines.


"Majukumu ya Kituo cha PPP ni pamoja na kuratibu na kuchambua miradi yote ya uwekezaji wa ubia kati sekta ya umma na sekta binafsi," Kafulila amesema.


Tanzania inakabiliana na changamoto kadhaa kwenye eneo la ubia PPP katika miradi ya kusafirisha umeme, ikiwemo masuala ya kanuni, sheria na upungufu wa uzoefu na utaalamu husika kwenye baadhi ya taasisi za umma.


Kuna haja ya taasisi za umma na watumishi wa umma kujengewa uwezo ili serikali iweze kushiriki kikamilifu kwenye ubia PPP ndani ya sekta ya nishati.


Baadhi ya wadau wa maendeleo wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa miradi ya ubia PPP kwenye ujenzi wa njia za kusafirisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya.


"Uzoefu wa wachumi wa nishati unaonesha kuwa sekta ya nishati inaweza kujitegemea kujiendesha yenyewe kifedha iwapo bei ya umeme itapangwa kibiashara," Kafulila aliongeza.


"Tanzania inauza umeme kwa bei ndogo kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, ndiyo maana Tanzania inaongoza kuwa na uchumi jumuishi kwenye eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara."


Wizara ya Nishati ilitangaza mwaka 2022 kuwa Serikali inahitaji Dola za Marekani bilioni 1.9 (zaidi ya Shilingi trilioni 5) ili kuimarisha njia za kusafirisha umeme nchini.


Tanzania kwa sasa inazalisha umeme wa ziada lakini inashindwa kuusafirisha umeme huo wa ziada kwenda kwenye maeneo ndani na nje ya nchi yenye uhaba wa umeme kutokana na upungufu wa njia za kusafirisha umeme.


Kafulila amesema kuwa ubia PPP kwenye ujenzi wa njia za kusafirisha umeme utaleta manufaa makubwa kwenye uchumi wa taifa.


Hii ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa umeme kwenye maeneo mengi zaidi nchini kwa gharama nafuu na kuchochea uchumi wa viwanda.

Previous Post Next Post