SHINYANGA: ASHRAPH MAJALIWA ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UENYEKITI WA MTAA WA VIWANDANI

Ashraph Majaliwa anayetarajia kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Viwandani kupitia chama cha mapinduzi.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Ashraph Majaliwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwandani kwa kipindi cha miaka mitano, amechukua rasmi fomu ya kugombea tena nafasi hiyo ili kuendelea kuwatumikia wananchi wa mtaa huo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na Misalaba Media mara baada ya kuchukua fomu, Majaliwa ameahidi kudumisha mshikamano, umoja, na kufanya kazi kwa bidii, akiwahakikishia wakazi wa Viwandani kuwa malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan yatatekelezwa kikamilifu kwenye mtaa huo.

 Aidha, ameahidi kuendelea kutoa fursa za ajira kwa wakazi kupitia viwanda vidogo vilivyopo Viwandani, kwa lengo la kusaidia vijana na wakazi ambao bado hawana ajira.

"Nimechukua fomu leo kugombea uenyekiti wa mtaa huu wa Viwandani mimi na timu yangu tuko tayari kushirikiana na mama yetu Rais Samia kuhakikisha miradi yote inayokuja inaleta manufaa kwa wananchi kama ilivyokusudiwa," amesema Majaliwa kwa kujiamini.

Ameongeza kuwa viwanda vya kuchakata mazao vilivyopo kwenye mtaa huo vitatumiwa kwa manufaa ya wakazi wote, hasa kwa wale ambao hawana ajira za kudumu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mjini, Mhe. Gulamhafeez Abubakari, amepongeza wananchi na wanachama wa CCM kwa kuwapa sapoti wenyeviti wao katika zoezi la uchukuaji wa fomu kwenye mitaa yote minne ya kata hiyo.

Ameeleza kuwa chama kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi, huku akiwataka wakazi wa kata ya Mjini kuwa na imani na wagombea wao.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 unatarajiwa kufanyika Novemba 27, ambapo wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji, na wajumbe wao watachaguliwa rasmi kwa muhula ujao wa uongozi.


 

Previous Post Next Post