SHINYANGA: CHADEMA KATA YA MJINI WAGOMBEA WARUDISHA FOMU, WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA NOVEMBA 27, 2024


Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya mjini, Bwana Nicholaus Luhende, akizungumza na Misalaba Media leo Oktoba 31, 2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kata ya Mjini jimbo la uchaguzi Shinyanga mjini, kimetoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi ifikapo Novemba 27, 2024 ili kuchagua viongozi wanaowataka.

Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya mjini, Bwana Nicholaus Luhende, ametoa wito huo leo wakati akizungumza na Misalaba Media baada wagombea nafasi ya mwenyekiti kutoka mitaa mbalimbali kurudisha fomu zao.

Kwa mujibu wa Luhende, wagombea wa CHADEMA katika mitaa miwili kati ya minne wamekamilisha zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za kugombea nafasi za wenyeviti wa mitaa na wajumbe.

"Tumefanikiwa kurudisha fomu katika mitaa yote ambayo tumepanga wagombea wito wangu kwa wananchi ni kuwa CHADEMA tumewaandaa wagombea wenye sifa na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa ufanisi," amesema Luhende.

Luhende amewahimiza wananchi kuzingatia umuhimu wa kupiga kura kwa viongozi wanaoamini katika maendeleo na wenye dhamira ya kuleta mabadiliko.

“Wananchi kwa sasa wanatambua tofauti kati ya uongozi bora na ule ambao umekuwa na changamoto  tunawataka wajitokeze kwa wingi na kuchagua viongozi wa kweli,” amesema Luhende.

Aidha, wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Buzuka Thomas Gumalija Machibya na Mkasha John Emmanuel wa mtaa Viwandani, ambao tayari wamerejesha fomu zao, wamesema kuwa hawajakumbana na changamoto yoyote katika hatua ya kuchukua na kurudisha fomu.

Wametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha uwazi na haki katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Zoezi la kurejesha fomu linatarajiwa kufikia tamati kesho, Ijumaa, Novemba 1, 2024, huku uchaguzi wa serikali za mitaa ukipangwa kufanyika rasmi Novemba 27, 2024.

Siku hiyo, wananchi watapata nafasi ya kuchagua wenyeviti wa mitaa, vijiji, na vitongoji katika maeneo mbalimbali ya nchi.



 

Previous Post Next Post