SHINYANGA: SHIRIKA LA UZAO WETU LAJIKITA KATIKA MALEZI YA KIPAJI KAMA NJIA YA KUPUNGUZA UKATILI DHIDI YA WATOTO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la Uzao Wetu limewahimiza wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika mazingira bora yanayoendana na vipaji vyao ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili vinavyozidi kuongezeka.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Yusuph Mtobela, baada ya kutoa semina kwa walimu wa watoto katika Kanisa la Baptist Ngokolo, mjini Shinyanga na kwamba Semina hiyo ililenga kuwapa walimu hao elimu juu ya mbinu bora za kuwafundisha watoto malezi yanayokuza vipaji.

Mtobela amesema kuwa vitendo vya ukatili vinaongezeka kutokana na ukosefu wa malezi bora ndani ya familia na jamii ambapo ameomba ushirikiano wa karibu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto.

Ameendelea kueleza kuwa, malezi jumuishi ni muhimu kwa watoto kwani yanawapa nafasi ya kukua wakiwa na uelewa mzuri wa uwezo wao ambapo amesema kuwa shirika lake linaamini kuwa malezi bora yatakayoitikia kipaji ni njia madhubuti ya kupunguza vitendo vya ukatili na kuhakikisha watoto wanalelewa katika njia sahihi.

“Uzao wetu tunashughulika sana na masuala ya ulinzi wa mtoto katika nyanja zote lakini tumejikita kwenye malezi yanayoitikia kipaji kama silaha moja ya ulinzi na usalama wa mtoto kwa sababu mtoto ukimlea kulingana na kipaji chake atakuwa na uwezo wa kujitetea lakini pia malezi ya kipaji na malezi jumuishi ni lazima watoto wakae pamoja kwa ujumla tunasema malezi ya watoto ni malezi ya jamii”.

“Malezi mazuri ambayo kwa sasa hivi watu wengine wanasema haiwezekana mimi nakwambia inawezekana malezi yanayoitikia kipaji ni malezi yatakayotutoa kwenye ukatili wa aina yoyote ninaimani ya kwamba kila siku mungu anapotujalia uzima tunaweza kushirikiana na kila mtu ambaye yuko kwa ajili ya ulinza na usalama wa mtoto”.amesema Mtobela

“Ili watoto wawe salama na wenye ustawi mzuri, ni lazima wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla washirikiane kwa dhati katika kuwapa malezi yanayoendana na vipaji vyao”.

Katika semina hiyo, mwalimu wa watoto kutoka Kanisa la Baptist Ngokolo, Jackson Kalijeje, ameelezea umuhimu wa kufuata mafundisho ya kidini kama msingi wa malezi bora kwa watoto huku akirejea maandiko ya Biblia, alisema mafundisho hayo yanawapa wazazi na walezi mwongozo wa jinsi ya kumlea mtoto katika njia ipasayo.

“Kitabu cha Methali 22:6 kinasema, 'Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee,'” amesema Kalijeje, ambapo ameongeza kuwa kanisa hilo limeona upungufu mkubwa wa malezi katika jamii, hasa kwa watoto, hivyo wamechukua jukumu la kuwaelimisha wazazi na walezi ili kuhakikisha watoto wanalelewa kwa kufuata njia sahihi.

Kalijeje alifafanua kuwa kanisa lao limekuwa na ushirikiano wa karibu na Shirika la Uzao Wetu katika kuwafundisha watoto ndani ya kanisa na jamii inayowazunguka na kwamba ushirikiano huo umeanza kuzaa matunda ambapo mafundisho yaliyotolewa yanaanza kuonyesha matokeo chanya katika malezi ya watoto.

 “Tumeona kuna upungufu mkubwa sana wa malezi kwa watoto wetu hivyo sisi kama kanisa la Baptist tulina neno la Mungu katika kitabu kile cha Methali sura ya 22 mstari wa 6 inasema mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee”.

“Tuliona kumbe kuna nafasi kubwa sana ya mzazi, kanisa na jamii kumlea mtoto, katika sehemu hiyo sasa sisi kama kanisa ikatusukuma mbele zaidi kuangalia ni namna gani tunaweza kushughulika na watoto waliomo ndani ya kanisa na jamii inayotuzunguka tulilipata kanisa la Uzao wetu kwa lengo la kushirikiano nalo kwa sasa tumepiga hatua sana tumeanza kuyaona matokeo kupitia mafundisho ambayo tunayatoa kwa kushirikiana na shirika la Uzao wetu”.amesema Kalijeje

Walimu waliohudhuria semina hiyo wamelipongeza na kulishukuru Shirika la Uzao Wetu kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ambapo wamesema  kuwa elimu hiyo imewawezesha kufahamu mbinu bora za kuwalea watoto kwa njia zinazokuza vipaji vyao, na hivyo kuwasaidia kuwa na uwezo wa kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili na madhara mengine yanayoweza kuwapata.

Baadhi ya walimu walioshiriki semina hiyo walieleza furaha yao kwa kupata fursa hiyo na wakaahidi kuwa mabalozi wa kueneza elimu hiyo kwa wazazi na walezi katika maeneo yao, ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye manufaa kwa mustakabali wao.

Shirika la Uzao Wetu limeendelea na juhudi zake za kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yanayokuza vipaji vyao, hatua ambayo inatajwa kuwa muhimu katika kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.

Ujumbe wa Mkurugenzi wa Uzao Wetu na mwalimu wa Kanisa la Baptist umesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, jamii, na taasisi za kidini katika kuwasaidia watoto kuwa na malezi bora.

Aidha katika semina hiyo walimu wa watoto wamefundishwa nyimbo na michezo mbalimbali ya watoto.


Mkurugenzi wa Shirika hilo, Yusuph Mtobela akitoa elimu kwa walimu wa watoto kanisa la Baptist kuhusu malezi yanayokuza vipaji kwa watoto.

Mwalimu wa watoto kutoka Kanisa la Baptist Ngokolo, Jackson Kalijeje, akifundisha.


TAZAMA VIDEO 2

Previous Post Next Post