SHINYANGA: WAGOMBEA CHADEMA KATA YA NDEMBEZI WAMERUDISHA FOMU ZA UONGOZI MITAA, WAJIANDAA KWA UCHAGUZI TAREHE 27 NOVEMBA

Katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika tarehe 27 Novemba, wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, wameanza maandalizi kwa kurudisha fomu za kugombea nafasi za uongozi katika mitaa mbalimbali ya kata hiyo.

Zoezi la kurejesha fomu linaonesha kuimarika kwa demokrasia ya upinzani miongoni mwa vyama vya siasa, huku wagombea wakionyesha utayari wao kushiriki katika uchaguzi na kuleta mabadiliko kwenye maeneo yao.

Miongoni mwa wagombea waliorejesha fomu ni Rodgers Robinson Mshana anayewania nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukareli, Abdallah Sube anayewania nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Mbuyuni, Jumanne Frank Maziku mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Mtaa wa Ndembezi, Titus Maris Jilungu (Mtaa wa Dome), Philimon Allan Nkonjwa (Mtaa wa Mabambase), na Steven James (Mtaa wa Butengwa).

 Akizungumza na Misalaba Media baada ya wagombea kurejesha fomu, Katibu wa CHADEMA Kata ya Ndembezi, Joseph Isack, amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa ufanisi na uangalifu mkubwa.

“Tulichukua fomu salama na leo tumerudisha salama, tumezijaza vizuri kwa umakini sasa ni kwa maafisa wa tume ya uchaguzi kutenda haki kama Rais alivyosema kuwa tume ni huru sisi tumejipanga vizuri, lengo letu ni kupata ushindi kwenye mitaa yote,” amesema Isack.

Ameeleza kuwa chama kimejiandaa kikamilifu kushiriki katika kampeni na kuwafikia wapiga kura, huku akitoa wito kwa Tume ya Uchaguzi na maafisa wake kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na haki, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na viongozi wa kitaifa.

Uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mnamo tarehe 27 Novemba unalenga kuchagua viongozi wa mitaa, vijiji na Vitongoji nafasi ambazo zinajumuisha uenyekiti na wajumbe wa mitaa, vijiji na Vitongoji.

Uchaguzi huo ni muhimu kwani viongozi wanaochaguliwa wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kuendeleza miradi ya maendeleo na huduma kwa wananchi, ikiwemo afya, elimu, na miundombinu.

CHADEMA inatoa wito kwa wananchi wa Kata ya Ndembezi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo ili kuwachagua viongozi wanaoamini kuwa watasimamia maslahi yao.

Pia, chama hicho kinasisitiza umuhimu wa kulinda amani wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi.

Kama ambavyo wagombea wa CHADEMA walivyorejesha fomu na kujipanga kuanza kampeni, macho yote yanaelekezwa kwenye tarehe 27 Novemba, siku ambayo wananchi wa mitaa mbalimbali watapiga kura kuchagua viongozi wao.

Titus Maris Jilungu mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Mtaa wa Dome akirudisha fomu leo Oktoba 30, 2024.

Philimon Allan Nkonjwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Mtaa wa Mabambase akirudisha fomu leo Oktoba 30, 2024.



 

Previous Post Next Post