SHINYANGA: WAGOMBEA SITA WA CCM NDEMBEZI WAMECHUKUA FOMU ZA KUGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI KWENYE MITAA YAO

Na Mapuli Kitiba Misalaba

Katika hatua muhimu kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wagombea wa nafasi ya mwenyekiti kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mitaa sita ya kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, leo wamechukua rasmi fomu za kugombea.

Zoezi hilo limeambatana na maandamano ya amani, ambapo wagombea wametembelea mtaa kwa mtaa, wakipokea sapoti kutoka kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho.

Wagombea hao ni pamoja na Onesmo Mahenda Ruhende anayewania nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Butengwa, Mariam Mikidadi Mdoe anayegombea mtaa wa Ndembezi, Bakari Juma kutoka mtaa wa Mabambase, Seif Nassor Hamed wa mtaa wa Mbuyuni, Tabitha Costantine Shilingi wa Tambukareli, na Solomon Nalinga Najulwa ambaye anagombea tena nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Dome ambapo kila mmoja wao anagombea kwa tiketi ya CCM.

Akizungumza na MISALABA MEDIA, katibu wa CCM kata ya Ndembezi, Pendo Sawa, ameelezea furaha yake kuhusu kujitokeza kwa wanachama wa chama hicho katika kuwasindikiza wagombea wao.

"Leo wenyeviti wetu waliopita kwenye kura za maoni ndani ya chama wamejitokeza kuchukua fomu. Nawaomba wanachama, wapenzi, na wakeleketwa wa CCM waungane nasi kesho wakati wa kurudisha fomu," amesema Pendo Sawa.

Katibu Mwenezi wa CCM kata ya Ndembezi Issa Said Stima, amesisitiza kuwa chama kimejipanga vema kwa ajili ya uchaguzi huo huku akionyesha kujiamini kuhusu ushindi wa wagombea wao.

 "CCM tumejipanga kwenye uchaguzi tunawaomba wenzetu wasikimbie na mpira makwapani sisi tuko tayari kuingia majukwaani," amesema Stima.

Zoezi la kuchukua fomu limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM, ikiwemo Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Said Sakala, pamoja na katibu wa UVCCM Wilaya hiyo, Naibu Katalambullah.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, ambapo wananchi watapata nafasi ya kuchagua viongozi wao wa mitaa, vijiji, vitongoji, na wajumbe wao.

Hii ni nafasi muhimu kwa wananchi kushiriki katika uongozi na maendeleo ya maeneo yao.

Awali wakati wa maandamano ya amani mtaa kwa mtaa.



Solomon Nalinga Najulwa ambaye anagombea tena nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Dome kupitia chama cha mapinduzi CCM, akikabidhiwa fomu yake leo Oktoba 29, 2024.

Solomon Nalinga Najulwa ambaye anagombea tena nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Dome kupitia chama cha mapinduzi CCM, akikabidhiwa fomu yake leo Oktoba 29, 2024.

 

Previous Post Next Post