POLISI SHINYANGA WAMKAMATA MTU KWA KUFYATUA RISASI BAADA YA MZOZO

Na Mapuli Kitina Misalaba 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limemkamata mtu mmoja kwa kosa la kufyatua risasi mbili kwa kutumia bastola aina ya BROWNING 9mm. 

Tukio hilo lilitokea katika baa inayojulikana kama Lubaga Inn iliyopo ndani ya Manispaa ya Shinyanga usiku wa tarehe 24 Oktoba, 2024, majira ya saa mbili ambapo Mtu huyo, ambaye bado hajatambulika rasmi, alifyatua risasi moja hewani na nyingine akielekeza kaunta ya vinywaji, ingawa chanzo cha mzozo huo hakijafahamika mpaka sasa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Shinyanga, Kennedy Mgani, ameeleza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika. 

Jeshi la Polisi limewatoa hofu wananchi kwa kuahidi kuhakikisha usalama na kutekeleza taratibu zote za sheria husika dhidi ya umiliki na matumizi ya silaha.

Katika taarifa nyingine iliyotolewa na Polisi tarehe 23 Oktoba 2024, kuhusu operesheni ya ukamataji wa watu waliojihusisha na biashara haramu, Polisi ilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 14 na bidhaa mbalimbali zilizohusishwa na makosa ya biashara haramu. 

Miongoni mwa bidhaa hizo ni pamoja na pombe ya moshi (pombe za kienyeji) 87, gari moja aina ya Scania, redio tano, pikipiki tano, mashine za kufanyia kazi mbili, godoro mbili, na chupa 23 za pombe aina ya Hanson Choice.

Kuhusiana na pombe hizo aina ya Hanson Choice, Polisi imekanusha vikali madai ya kuwa bidhaa hizo ni feki au zilizoingizwa nchini kinyemela. 

Uchunguzi umebaini kuwa pombe hizo zimetengenezwa na kiwanda halali na zina stika sahihi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hata hivyo, uvumi huo ulisambaa baada ya watu waliodai kuporwa kuzusha maneno mitandaoni wakidai kuwa bidhaa hizo ni za magendo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limetoa wito kwa wamiliki wa silaha kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu zote za umiliki ili kuepusha matatizo yoyote yanayoweza kujitokeza. 

Aidha, Polisi imewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa na kusisitiza kuwa kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha usalama wa mkoa unaendelea kudumishwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Kennedy Mgani, amesisitiza kuwa Polisi haitasita kumchukulia hatua kali mtu yeyote atakayekiuka taratibu za umiliki wa silaha, ikiwa ni pamoja na kumnyang'anya silaha kwa mujibu wa sheria.



Previous Post Next Post