Na Mapuli Kitina Misalaba
Msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa, Mwalimu
Alexius Kagunze, ameendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye
zoezi la uandikishaji wa wakazi.
Zoezi hilo limeanza rasmi tarehe 11 Oktoba 2024, na
litafikia tamati tarehe 20 Oktoba 2024, likiwa na lengo la kuwaandikisha wapiga
kura watakaoshiriki uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.
Kagunze ameeleza kuwa, zoezi hilo linaendeshwa kila
siku kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, na hakuna muda wa
ziada utakaongezwa baada ya siku kumi zilizotengwa.
“Naendelea
kuwasihi wananchi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kufika kwenye
vituo vilivyo karibu na makazi yao ili waweze kujiandikisha. Hili ni zoezi
muhimu sana, na kama hukutumia fursa hii, utapoteza haki ya kushiriki kwenye
uchaguzi wa tarehe 27 Novemba 2024. Sifa kuu za kujiandikisha ni kuwa na umri
wa miaka 18 na kuendelea, pamoja na kuwa mkazi wa eneo husika,”
amesema Kagunze.
Naye Katibu wa jumuiya ya shujaa wa maendeleo na
ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Daniel Patrick Kapaya
ameendelea kuhamasisha wananchi, hususan vijana wa mikoa ya Shinyanga, Mwanza,
Mara, Simiyu, Geita, na Kagera, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.
“Naomba
sana mashujaa wote wa kanda yangu ya Ziwa, pamoja na wananchi kwa ujumla,
wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wakazi. Ni haki ya msingi kwa kila
mmoja kujiandikisha ili aweze kupiga kura, kwani usipojiandikisha unajinyima
haki hiyo. Tarehe 27 Novemba 2024, tutakuwa na uchaguzi wa viongozi wa serikali
za mitaa, ambao ndio watahakikisha maendeleo ya mitaa yetu,”
amesema Kapaya.
Kapaya ameendelea kufikisha salamu za mwenyekiti wa
taifa wa SMAUJATA, Sospeter Bulugu, akisisitiza kuwa mashujaa na wananchi kwa
ujumla wanatakiwa kujitokeza ili kujiandikisha ambapo amewasisitiza wananchi
wasikose fursa hiyo kwani ndio itakayowezesha ushiriki wao katika uchaguzi wa
viongozi watakaoliongoza taifa kwa ngazi za mitaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Idara ya Itifaki,
Uenezi, na Uanachama wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Solomon Najulwa, ameungana
na viongozi wenzake kutoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuhakikisha
wanajiandikisha kwa wingi.
Najulwa amesema kuwa, zoezi hilo ni tofauti na ule
wa kuboresha daftari la wapiga kura ambalo litatumika mwaka 2025 kwenye
uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, na rais.
“Zoezi
hili ni la uandikishaji kwenye daftari la wakazi, halihusishi kitambulisho
chochote. Unachotakiwa ni kutoa majina yako matatu, umri, na sahihi uandikishaji
huu ni wa haraka, na mara tu unapomaliza, unakuwa na sifa ya kuwa mkazi halali
wa eneo husika,” amesema Najulwa.
Najulwa amewahimiza wananchi, hususan wale wanaoishi
na watu wenye ulemavu au wazee, kuwasaidia kufika kwenye vituo vya uandikishaji
ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya kushiriki uchaguzi huo.
“Kama
hatutawasaidia ndugu zetu wenye ulemavu au wazee kufika kwenye vituo vya
uandikishaji, tutakuwa tunafanya ukatili kwa kuwanyima haki yao ya msingi SMAUJATA
tunasema, tuonyeshe upendo kwao kwa kuwahakikisha wanajiandikisha,”
amesema Najulwa.
Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa
utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024 ni mchakato muhimu kwa maendeleo ya maeneo
ya mitaa.
Viongozi watakaopatikana katika uchaguzi huo
watakuwa na jukumu kubwa la kusimamia maendeleo na ustawi wa jamii katika ngazi
za msingi ambapo Wananchi wanahimizwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa
kujiandikisha na kisha kushiriki uchaguzi huo.
Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa wamepewa mwaliko wa kutumia siku zilizobaki kuhakikisha wanajiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, kwani uandikishaji huu ni fursa ya kipekee kwao kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Katibu wa jumuiya ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Daniel Patrick Kapaya, akijiandikisha kwenye daftari la wakazi.
Mwenyekiti wa Idara ya Itifaki, Uenezi, na Uanachama wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Solomon Najulwa (Cheupe) akijiandikisha kwenye daftari la wakazi.