Ticker

6/recent/ticker-posts

SHINYANGA YAJIANDAA KWA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, WANANCHI WAHAMASISHWA KUJITOKEZA, VIONGOZI WA SIASA WATAKA AMANI NA HAKI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Zoezi la Uandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura Serikali za Mitaa 2024 katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shinyanga inajiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la uandikishaji wapiga kura, Mhe. Macha amesisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi bora watakaosaidia kuleta maendeleo ya mkoa.

Mhe. Macha amewaomba wakazi wa Shinyanga kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

"Tunahitaji viongozi watakaolinda rasilimali zetu na kusaidia miradi ya maendeleo, si wale mafisadi ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao," amesisitiza Macha.

Katika hotuba yake, amewahamasisha wanaume na wanawake wenye sifa kuwania nafasi za uongozi, huku akiwapongeza akina mama kwa kuonyesha mwamko mkubwa wa kushiriki.

"Akina mama wamechangamka sana safari hii, tunataka pia wanaume wasibaki nyuma Uchaguzi huu ni wa kila mmoja wetu," amesema.

Mkuu wa Mkoa amehakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa haki, huru, na wa amani, akiongeza kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha usalama unadumishwa kabla, wakati, na baada ya uchaguzi. "Tunataka uchaguzi huu uwe wa haki na amani hatutaki ugomvi au vurugu; kila mmoja ana haki ya kugombea lakini kwa njia ya amani," amesema.

Amewataka wagombea kufuata taratibu na sheria za uchaguzi, huku akiwahimiza wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura bila vitisho au ushawishi wa aina yoyote.

 Pia amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha ili waweze kuchagua viongozi wanaofaa na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura katika Manispaa ya Shinyanga litaanza rasmi tarehe 11 Oktoba 2024 na kumalizika tarehe 20 Oktoba 2024 na kwamba  lengo kuu ni kuandikisha wapiga kura 120,345 kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa, ikiwa ni pamoja na kata 17, vijiji 17, vitongoji 84, na mitaa 55.

Charles Dominic, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Manispaa ya Shinyanga, ametoa wito kwa wananchi kujiandikisha kwa wakati, akisisitiza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa uwazi na haki.

Vituo vya uandikishaji vimewekwa katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kila mkazi ana fursa ya kujiandikisha bila usumbufu.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Elias Masumbuko, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hii ya kujiandikisha ili waweze kushiriki katika uchaguzi.

"Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunaongoza kwa kushiriki na kuchagua viongozi wanaotufaa kwa maendeleo yetu ya baadae," amesema Masumbuko.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa mkoani Shinyanga wamehimiza kufanyika kwa uchaguzi wa haki, huru, na wa amani, wakisisitiza kuwa hili ni jambo muhimu kwa maendeleo ya jamii.

Wakizungumza na Misalaba Media, viongozi hao wamesema kuwa uchaguzi huru na wa haki ndio msingi wa demokrasia na ustawi wa taifa, hivyo ni muhimu wananchi wahakikishiwe mazingira salama na ya uwazi wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Viongozi hao wameongeza kuwa, ili kufanikisha uchaguzi wa amani, vyama vya siasa vinatakiwa kuepuka ghasia na uchochezi, na badala yake kuzingatia hoja za maendeleo na sera zinazolenga kuboresha hali za wananchi.

Wakisisitiza umuhimu wa amani, viongozi hao wameeleza kuwa, bila uchaguzi wa amani, maendeleo ya kijamii na kiuchumi hayawezi kufikiwa.

Baadhi ya wananchi wa wa Manispaa ya  Shinyanga wamesema wanatambua umuhimu wa kushiriki katika hatua muhimu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, wakisema kuwa mchakato huu unatoa fursa kwa kila mmoja kumchagua kiongozi bora mwenye uwezo wa kutatua changamoto za jamii.

 Wameeleza kuwa kwa kuchagua viongozi wenye sifa, watakuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya kweli katika maeneo yao.

Aidha, wananchi hao wameomba kuendelea kutolewa kwa elimu ya mpiga kura ili kuwasaidia kuelewa vizuri umuhimu wa kushiriki katika hatua zote za uchaguzi.

Wamebainisha kuwa elimu hiyo itasaidia wananchi kujua haki na wajibu wao, kuanzia kwenye hatua ya kujiandikisha hadi kushiriki mikutano ya hadhara, jambo ambalo litawasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.

Wakizungumza na Misalaba Media, wananchi hao wamehimiza viongozi wa serikali na wadau wengine kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi, ili kuongeza hamasa na uelewa kwa wapiga kura.

Wamesema, bila uelewa wa kutosha, itakuwa vigumu kwa wananchi kuchagua viongozi wanaoweza kutatua changamoto zinazowakabili, hivyo ni muhimu elimu hiyo imfikie kila mmoja.

Mkoa wa Shinyanga uko tayari kwa uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024, ambapo wananchi wanaendelea kuhamasishwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki kikamilifu.

Uchaguzi huu unalenga kuweka viongozi bora watakaosukuma gurudumu la maendeleo mbele, huku usalama na amani vikihakikishwa kwa kila hatua.


Hafla ya uzinduzi wa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ikiendelea uwanja wa Saba saba Manispaa ya Shinyanga.

Hafla ya uzinduzi wa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ikiendelea uwanja wa Saba saba Manispaa ya Shinyanga.


 

TAZAMA VIDEO

TAZAMA VIDEO



Post a Comment

0 Comments