WAGOMBEA CHADEMA KATA YA NDALA WAMERUDISHA FOMU MITAA YOTE 5 WASISITIZA UCHAGUZI WA HAKI NA UWAZI

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Katika jitihada za kuimarisha demokrasia katika ngazi ya mitaa, wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe wao kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga leo wamerudisha fomu zao rasmi.

Katika mtaa wa Banduka mgombea ni Stella Steven Kyaruzi,  John Robert Shindayi mgombea katika mtaa wa Mlepa,  Robert Chacha Rhobi mgombea katika mtaa wa Mapinduzi,  Benjamin Shija Salaganda mgombea wa mtaa wa Ndala pamoja na Suleiman Said mgombea katika mtaa wa Mwabubndu kupitia CHADEMA.

Wakizungumza na Misalaba Media, wagombea hawa wameonyesha furaha yao kwa jinsi zoezi la kurudisha fomu lilivyoendeshwa kwa utulivu na usalama.

Katibu wa CHADEMA kata ya Ndala, Bw. Yusuph Juma Nkubana, ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa.

"Wananchi mmewaona wagombea wetu, rai yangu ni kwamba hatua zote za uchaguzi zifanyike kwa utaratibu sahihi. Hatutakubali aina yoyote ya udanganyifu," amesema Nkubana kwa msisitizo.

Bw. Nkubana amewaomba wasimamizi wa uchaguzi kuwa waangalifu na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi na uaminifu ambapo ameongeza kuwa utekelezaji wa taratibu za uchaguzi utawezesha wananchi kupata viongozi wanaowahitaji, na kwamba CHADEMA haitavumilia mapungufu yoyote katika uchaguzi huu.

Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Ndala, Bw. Enock Mpyalimi Makondu, amesisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka huu unapaswa kuwa wa uwazi na usawa.

 “Rai yangu kwa tume ya uchaguzi ni ifanye kazi kwa uwazi na ukweli hatutaki kusikia mtu anapitishwa bila ushindi wa kura nyingi wananchi wanastahili kupata viongozi wanaowahitaji, na kwa haki hiyo ni lazima uchaguzi ufanyike kwa utulivu na amani.”amesema Makondu

Makondu amewahimiza wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha kwamba matokeo yanatangazwa kwa uhalisia, kwa kuzingatia kura halisi za wananchi, na siyo kwa upendeleo wa aina yoyote.

Afisa mipango na uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Bw. Joseph Ndatala, amehudhuria tukio hilo na kutoa wito wa kuendeleza mazingira ya uchaguzi wa haki na uwazi.

 “Hakuna eneo lililobaki bila mgombea haki ya uchaguzi katika hatua hii ni nzuri sana, lakini tunasisitiza zoezi liendelee kuwa la haki tukiona mabadiliko yasiyo ya haki, CHADEMA itachukua hatua kwa vitendo” amesema Ndatala kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi, CHADEMA imekuwa ikiomba uchaguzi wa haki na uwazi kwa kauli, lakini safari hii wapo tayari kuchukua hatua zaidi ikiwa changamoto zitatokea.

Misalaba Media itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchaguzi huu na kutoa taarifa za kina kwa wananchi.

Stella Steven Kyaruzi mgombea wa nafasi ya mwenyekiti mtaa wa Banduka kupitia CHADEMA akirudisha fomu yake.

Stella Steven Kyaruzi mgombea wa nafasi ya mwenyekiti mtaa wa Banduka kupitia CHADEMA akirudisha fomu yake.

Benjamin Shija Salaganda mgombea wa nafasi ya mwenyekiti mtaa wa Ndala akirudisha fomu leo Oktoba 20, 2024.

 

Previous Post Next Post