NA LUCAS RAPHAEL,TABORA
Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) imeingia makubaliano na
wakulima wa mkataba zaidi ya 80 watakiwa kuzalisha Mbegu bora za kilimo kutoka tani 2,400 hadi kufikia tani 7,000 za mazao mbalimbali katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA ,Leo Mavika wakati akifungua cha makubaliano ya Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo kilichofanyika octoba 17 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Edema mkoani Morogoro.
Alisema kwamba moja ya majukumu ya Wakala wa Mbegu za kilimo ni kufanya kazi na Taasisi Binafsi na kuongeza Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo hadi kufia tani 7,000.
Leo alisema makubaliano hayo yatawekwa kisheria ili kila pande kuwepo na makubaliano ambayo yanalenga kuongeza Uzalishaji wa Mbegu.
Alibainisha kuwa wakala itazingatia na kufuatilia kila kipengele katika mikataba ili kuhakikisha kila upande unawajibika ipasavyo ambapo lengo ni kuongeza tija katika Uzalishaji.
Kaimu Mtendaji huyo aliendelea kusema baadhi ya wakulima wa mkataba wamekuwa na kasumba ya kuchukua maeneo makubwa na kushindwa kulima hali inayopelekea Taasisi kutofikia malengo kama ilivyotarajiwa.
Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa na kasumba ya kutosimamia mashamba yao pindi wanapoingia shambani hali hii pia inayopelekea Taasisi kupata hasara nakutofikia Malengo ya Uzalishaji.
Alisema wakulima hao wa mkataba wanapaswa kutambua Uzalishaji wa Mbegu ni tofauti na uzalishaji wa chakula hivyo kupitia wataalamu wa ASA wadau hawa watapewa maelezo sahihi pamoja na kuendelea kushauriwa wakati wa zoezi la uzalishaji mbegu mashambani.
Leo aliwataka wakulima hao kuwa makini katika Uzalishaji wa Mbegu kwani Taasisi hiyo unaweka Malengo ya serikali pamoja na wakulima kutegemea Mbegu hizo ziwafikie sokoni kwa wakati na ubora uliokusudiwa
"Tunataka tuwe makini katika Uzalishaji wa Mbegu hatutaki mzaha mzaha kwani serikali imetupa malengo hivyo ni matumaini yetu mtafanya kazi vizuri pasipo kuwa na changamoto zozote." alisema Leo
Akitoa ufafanuzi wa kisheria mwanasheria wa Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA Valentine Kamugisha alisema lengo la Kikao hicho ni kuwaweka pamoja wakulima wa mkataba na kuwapatia mikataba ili wazalishe mbegu kwa kufuata utaratibu madhubuti wa kisheria.
Alisema Wakala inatarajia kuona matokeo chanya ya Uzalishaji wa Mbegu kuwa makubwa na ya kisasa kutokana na kuingia mikataba ambayo itaweka usawa kati ya Wakala na mkulima.
Aidha alisema baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya udokozi wa Mbegu na kuuza Mbegu kama chakula hali inayopelekea Taasisi kupata hasara yakutopata Mbegu kulingana na makadirio yaliyowekwa
Alisema Wakulima wakiwa waaminifu watapewa nafasi ya kulima kila wakati kutokana na historia ya mkulima husika ambayo haina usumbufu.
Valentine alisema kuwa mkulima haruhusiwi kukodisha Shamba alilopewa na Wakala kwa ajili ya Uzalishaji pamoja na kuuza mavuno sehemu nyingine tofauti na mkataba unavyomtaka.
"Tunachowaomba kuzingatia mikataba hii haruhusiwi kukodisha ama kuuza Shamba la Wakala na kama ukizalisha Mbegu huruhusiwi kuuza kama Mazao ya chakula nawaomba mzingatie mikataba hii kama mtu akikiuka hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake." alisema mwanasheria Valentine Kamugisha.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Dkt. Justin Ringo alisema Wakala wa Mbegu ina matumaini makubwa na wakulima hao wa mkataba katika zoezi hilo la Uzalishaji wa Mbegu.
Alisema matarajio ya Wakala wa Mbegu kuwa wakulima hao wazalishe zaidi ya Tani 7,000 za Mbegu kwa Mazao mbalimbali.
Mkurugenzi wa Uzalishaji amewataka wakulima hao kutokuwa na kilimo cha mitandaoni badala yake watenge muda wa kutembelea Mashamba yao ilikuepuka hasara zinazoweza kujitokeza kwa kutotembelea Shamba.
Aidha Dkt. Ringo aliwataka wakulima hao kuzingatia kanuni za Uzalishaji wa Mbegu bora hasa kupanda na kuvuna kwa wakati, utunzaji mazao, usafi wa mbegu pamoja na uhifadhi kabla ya kusafirisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakulima wa mkataba wameipongeza Wakala wa Mbegu ASA Kwa kufanya kazi na wakulima wa mkataba juu ya Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo.
Mwambambale Asajile mkulima wa mkataba Shamba la Mbegu Kilangali alisema Kikao hicho cha wakulima na Wakala ni Kikao kizuri kinacholenga kuimarisha ushirikiano wa Uzalishaji wa Mbegu ili kuongeza Uzalishaji Nchini.
Alisema Wakulima hao watafanya kazi kwa kuzingatia mikataba inavyosema ili kufikia Malengo na kuongeza kuwa Wakala wa Mbegu unapaswa kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyoainishwa na wakulima hao.
Kikao hicho kimefanyika kikiwa na lengo la kuhakikisha wakulima hao wanaingia mkataba na Wakala wa kuzalisha Mbegu bora kwa kufuata taratibu na kanuni za Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo.