Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Visiwani Zanzibar kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Balozi Omari Ramadhan Mapuri wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA kisiwani Pemba leo Oktoba 2, 2024.
Amewahimiza
watendaji hao kuwahamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kujiandikisha na
kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi
wao.
“Ni
matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa
wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania” amesema Mhe. Balozi Mapuri.
Kwa upande
wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira amewataka
watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki
kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
“Mabango na
vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika shehia zote zilizopo katika
mikoa yote mitatu ya Unguja. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli
zote za uboreshaji katika shehia zote” amesema Mhe. Magdalena.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura visiwani Zanzibar umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 13 Oktoba, 2024 ambapo katika Ksiwa cha Pemba utafanyika katika mikoa miwili na Unguja katika mikoa mitatu.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya mazoezi ya vitendo ya matumizi ya mashine za BVR ambazo zitatumika kusajili Wapiga Kura visiwani Zanzibar katika zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotaraji kuanza Oktoba 7 hadi 13 mwaka huu.Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya mazoezi ya vitendo ya matumizi ya mashine za BVR ambazo zitatumika kusajili Wapiga Kura visiwani Zanzibar katika zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotaraji kuanza Oktoba 7 hadi 13 mwaka huu.