ZIARA YA KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA WAZAZI ALLY HAPI AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO ISAKA NA JANA, KAHAMA MKOANI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Mhe. Ally Hapi, Oktoba 1, 2024 ameanza ziara yake  Mkoani Shinyanga kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kata za Isaka na Jana, Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama.

Katika ziara hiyo, ameambatana na viongozi wa chama na serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi.

Mhe. Hapi ametembelea Shule ya Sekondari Jana, ambapo amezungumza na wananchi na kuwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu huku akiwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ya kitaaluma.

Pia, Mhe. Ally Hapi amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu wa 2024.

Katika hotuba yake, Mhe. Ally Hapi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kuwaletea maendeleo Watanzania. "Tuna kila sababu ya kumshukuru Mhe. Rais kwa jitihada zake za dhati katika kuboresha maisha ya Watanzania ni muhimu tuendelee kumuunga mkono katika kuhakikisha maendeleo haya yanawafikia wananchi wote, hasa vijijini ambako miradi mingi ya kijamii na kiuchumi inatekelezwa kwa kasi kubwa," amesema Hapi.

Ziara hiyo ya Mhe. Hapi itadumu kwa siku sita, ambapo atatembelea majimbo yote katika Halmashauri 6 za mkoa wa Shinyanga, huku akifanya mikutano ya ndani na mikutano ya hadhara kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi.

Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. John Siagi amemshukuru rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi huku akimpongeza mbunge wa jimbo la Msalala Mhe. Iddi Kassim Iddi kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa ilani ya chama cha mapinduzi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Mhe. Ally Hapi, akipokelewa na viongozi baada ya kuwasili Mkoani Shinyanga kwa ajili ya ziara yake Oktoba 1, 2024.




 

Previous Post Next Post