Ticker

6/recent/ticker-posts

ZIARA YA WAZAZI USHETU: UCHAGUZI 2024 NA 2025 WAPEWA MSISITIZO, MNEC HAMOUD (MZEE WA SAMBUSA): "RAIS SAMIA NI KIONGOZI HODARI, AMELETA MABADILIKO YA KWELI"

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), maarufu kama Mzee wa Sambusa, Mhe. Hamoud Abuu Jumaa, amewahimiza wananchi kuendelea kuiamini na kuunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimbo la Ushetu, mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM, Mhe. Hamudi amesisitiza kuwa kwa maendeleo endelevu nchini, ni muhimu wananchi waendelee kuiunga mkono serikali ya chama hicho.

Mhe. Hamoud ameeleza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za wananchi, umekuwa na kasi zaidi katika serikali ya awamu ya sita.

"Watu wanasema Rais Samia anabahati, lakini bahati hiyo inatokana na vitendo vyake ameendelea kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na hayati Dkt. Magufuli kwa kasi kubwa, Rais Samia amejenga madaraja, viwanja vya ndege, ameendeleza miradi ya elimu bure na afya, na hata ujenzi wa reli ya mwendo kasi." Amesema Mhe. Hamoud

Mhe. Hamoud pia ameelezea jinsi Rais Samia alivyorahisisha usafiri na kuboresha uchumi wa nchi kwa kuongeza idadi ya watalii, akisema kwamba miradi hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa taifa.

Ameongeza kuwa serikali imeimarisha demokrasia nchini, huku akiwataka wananchi kutokubali kuathiriwa na wale wanaotumia uhuru huo vibaya kwa kumtukana Rais.

Katika ziara hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mhe. Hamudi Abuu Jumaa na viongozi wengine, wametembelea shule ya sekondari Chambo na kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana.

Mhe. Hamudi amewataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ya kitaaluma, huku akiwaonya kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi ambayo yanaweza kuathiri ndoto zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Thomas Miyonga, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, wamewasihi wanafunzi kuepuka makundi yenye tabia mbaya kama vile uvutaji bangi na ulevi, na kuwa mfano bora katika jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, amebainisha kuwa serikali imeboresha miundombinu katika sekta ya elimu ambapo amewataka wanafunzi kuendelea kuiunga mkono serikali kwa lengo la kufikia maendeleo ya kitaifa.

Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Chelehani, ameongeza kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo imekuwa ikitekelezwa kwa ushirikiano wa serikali na wadau mbalimbali.

Wanafunzi wa sekondari ya Chambo wameahidi kusoma kwa bidii na kuwa mabalozi wa shule hiyo na jamii kwa ujumla.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mhe. Edwin Peter Nyakanyenge, amewakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huku akiwasihi wananchi kuchagua viongozi bora kutoka CCM kwa ajili ya maendeleo zaidi.

Wananchi walioshiriki mkutano huo wameahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na Mbunge wa Ushetu, Mhe. Chelehani, kwa jitihada zao za kutatua changamoto zao.

Ziara ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM inaendelea mkoani Shinyanga, ambapo Oktoba 3, 2024 viongozi wametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kufanya mikutano ya ndani na mkutano wa hadhara katika jimbo la Ushetu Wilaya ya Kahama.



 

Post a Comment

0 Comments