Na. Brigitha Kimario- Serengeti
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Massana Mwishawa ameongoza wadau wa uhifadhi, wananchi, ndugu wa marehemu, marafiki, maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kuuaga mwili wa Askari wa Uhifadhi daraja la tatu CR III ARAFAT SAIDI MIYIMBA (27) aliyefariki kwa kukanyagwa na Tembo jana tarehe 09.11.2024 wakati akitekeleza majukumu yake ya kuwarejesha tembo hifadhini baada ya kuvamia kijiji cha Mrito wilayani Tarime.
Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi -TANAPA, Naibu Kamishna Mwishawa alisema kuwa kifo hicho cha ghafla kimeleta simanzi kubwa kwa TANAPA na wadau wa Uhifadhi nchini na ametoa pole kwa familia na watumishi wote wa Jeshi la Uhifadhi kwa kuondokewa na askari hodari na mchapakazi.
Aidha, shirika linatambua mchango wake
katika uhifadhi na sekta nzima ya utalii na itaendelea kuuenzi na kuuthamini. Pia Kamishna Mwishawa alitoa tahadhari kwa maafisa na askari kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka madhara na vifo vinavyoweza kusababishwa na wanyama hao.
Askari Arafat aliyejitolea maisha yake kulinda rasilimali hizo ameagwa leo tarehe 10.11.2024 katika uwanja mdogo wa ndege wa Fort Ikoma uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na baadae mwili wake kusafirishwa kuelekea kijiji cha Changarawe Mzumbe mkoani Morogoro kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.