Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, leo Jumatano tarehe 27.11.2024, amepiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa, katika kituo cha shule ya msingi Bugoyi "A" mtaa wa Mbuyuni Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga.
Askofu Sangu amekuwa wa kwanza kupiga kura mara tu baada ya kituo cha kupigia kura kufunguliwa majira ya saa 2:00 asubuhi.
Mara baada ya kupiga kura yake, Askofu Sangu amewahamasisha wananchi wote kutumia haki yao ya kidemokrasia kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka na ambao wanaamini kuwa watawaletea maendeleo na kubainisha kuwa, kujiandikisha peke yake bila kwenda kupiga kura hakuna maana yoyote.
Leo, wananchi wote kwa upande wa Tanzania bara, wanapiga kura kuwachagua viongozi wao wa Serikali za Mitaa, ambao ni Wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wao, ambapo katika Manispaa ya Shinyanga, jumla ya vyama 9 vimesimamisha wagombea.