ASKOFU SANGU AWAHIMIZA WANANCHI KUWA MACHO DHIDI YA CHUKI NA MGAWANYIKO WAKATI WA KAMPENI ZA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, ameongoza Misa Takatifu katika Parokia ya Mwamapalala, ambapo waimarishwa 250 wamepokea Sakramenti ya Kipaimara.

Katika mahubiri yake, Askofu Sangu amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kujinufaisha kwa shida za wengine, akisema kuwa mwenendo huo ni dhambi mbele ya Mungu.

Amehimiza waumini kuwa vyombo vya haki, upendo, na mshikamano badala ya kujinufaisha kwa mateso ya wengine.

"Wapo watu wanaotumia mahangaiko na shida za wengine kujinufaisha. Angalia wagonjwa hospitalini, pengine unataka kupata dawa, lazima utoe kitu. Wanajinufaisha kwa shida za wengine."

"Juzi hapa limeanguka lile jengo la Kariakoo. Watu wamejitokeza kuanza kuchangisha michango kwa udanganyifu, wakisema ni fursa. Hii ni dhambi kubwa mbele za Mwenyezi Mungu."amesema Askofu Sangu

Askofu Sangu ameendelea kuonya juu ya dhuluma zinazotokea katika maeneo mbalimbali ya kijamii, ikiwemo misiba na masuala ya mirathi akitaja kuwa ni lazima jamii ipambane na tabia hizo zinazoleta huzuni na maumivu kwa familia.

"Na hii ndiyo huwa inatokea hata kwenye misiba yetu. Wale wanaoiba rambirambi, wanachangisha kwenye daftari, daftari linazunguka, wanaiba rambirambi wakisema ni fursa. Tusijinufaishe na shida za wengine. Mbaya zaidi, mirathi ya watoto ikitoka, tunawadhulumu. Wajomba na ndugu wakubwa wanakuja kuchukua mali zote na kumwacha mama katika hali ya mahangaiko na huzuni kubwa. Watu wanajinufaisha na shida za wengine."

"Kamwe tusijinufaishe na shida za wengine. Tuwe chanzo cha furaha, amani, upendo, uvumilivu, utu wema, uaminifu, upole, na kiasi. Tuwe chombo cha umoja na upendo katika maisha yetu."amesema Askofu Sangu

Akizungumza kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, Askofu Sangu ameomba waumini kutumia nafasi hiyo kuendeleza mshikamano wa kitaifa kwa kuchagua viongozi waadilifu.

Amehimiza watu wote waliokwisha jiandikisha kuhakikisha wanapiga kura na kuwachagua viongozi watakaotetea maendeleo ya kiroho na kimwili.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuliombea taifa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo amehimiza waumini kuwa macho dhidi ya wale wanaopandikiza chuki na kuleta mgawanyiko katika jamii.

Amewashauri wananchi kuhudhuria kampeni za wagombea kwa umakini na kuwauliza maswali ya msingi badala ya kushabikia matusi au kashfa dhidi ya wagombea wengine.

"Wapendwa, najua tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. Ni nafasi ya pekee ya kuendelea kuliombea taifa letu liendelee kubaki katika umoja, upendo, na mshikamano. Umoja na mshikamano wetu wa Watanzania tuendelee kuudumisha, tukiongozwa na Mungu Roho Mtakatifu."

"Tuliombee taifa letu liendelee kustawi vizuri katika umoja, upendo, na mshikamano wetu kama Watanzania. Tukiongozwa na Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, na waandamizi wake wote, ili taifa letu liendelee kustawi kiroho na kimwili. Tujiepushe na wale ambao kauli zao na fikra zao ni za kutugombanisha Watanzania, kutuchonganisha, au kupandikiza chuki ndani ya jamii. Tuwe macho na watu hao, hasa kwenye kampeni zinazofanyika. Maandiko Matakatifu yanasema, tutawatambua kwa maneno na matendo yao."

"Twendeni kwenye kampeni zao, tuwasikilize, na tuwaulize swali moja tu: Utatufanyia nini? Siyo kuanza kusema, 'Yule ni mwizi.' Hapana! Swali letu la msingi ni kumuuliza, Utatufanyia nini hapa kwenye eneo letu?"

"Nawaalikeni wote mliokwisha jiandikisha mkapige kura. Muwachague viongozi watakaotetea maendeleo. Hatutaki wababaishaji. Tunataka watu watakaotuletea maendeleo ya kimwili na kiroho."amesema Askofu Liberatus Sangu

Katika ziara hiyo, Askofu Sangu pia ameweka mawe ya msingi katika miradi miwili muhimu ya Parokia ya Mwamapalala. Ameweka jiwe la msingi katika Kigango cha Ngeme na pia nyumba ya mapadre katika Kigango cha Mwalushu na kwamba miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kiroho kwa waumini wa maeneo hayo.

Askofu Sangu amesisitiza kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuwa sauti ya haki, upendo, na mshikamano katika jamii, huku akiwataka waumini wote kuwa mfano bora wa maadili na uadilifu kwa wengine.

Padre wa parokia ya Mwamapalala Betus Maduhu amemshukuru Askofu Sangu kwa ziara yake katika parokia hiyo.

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu.

Previous Post Next Post