CCM YAONGOZA MATOKEO UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA JIMBO LA SHINYANGA MJINI

Uchaguzi wa Serikali za mitaa umefanyika hii leo kwa upande wa Tanzania bara, huku katika Manispaa ya Shinyanga wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongoza.
Taarifa za awali ambazo zimethibitishwa na viongozi wa vyama vya upinzani zimebainisha kuwa, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimebeba viti vyote katika jimbo la Shinyanga mjini.
Viongozi waliokuwa wakipigiwa kura kupitia uchaguzi huo, ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wao.
Zoezi la upigaji wa kura limeripotiwa kuanza kwa wakati katika maeneo mengi, huku baadhi ya maeneo yakielezwa kuwa na wapiga kura wachache ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Kufuatia uchaguzi huo wa Serikali za mitaa, wagombea wa upinzani wamelalamikia kuwepo kwa dosari kadhaa, ikiwemo idadi ya kura zilizopigwa kuzidi idadi ya watu waliojiandikisha, baadhi ya watu kukamatwa ndani ya vituo wakiwa na kura ambazo tayari zimepigwa pamoja na watu kupiga kura zaidi ya mara moja.
Dosari nyingine ambazo zimelalamikiwa na upinzani ni kuwepo kwa baadhi ya masunduku yenye kura ambazo zimeunganishwa pamoja na kupigwa kura, ambapo pia baadhi ya fomu zenye orodha ya majina ya wapiga kura walizitilia mashaka kutokana na kutokuwa na namba.

 

Previous Post Next Post