Na
Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Emmanuel Ntobi, leo ameeleza misimamo na matarajio ya chama hicho katika kuelekea kwenye
kampeni za uchaguzi.
Katika hotuba yake, Ntobi amesisitiza umuhimu wa
kampeni za amani na uchaguzi ulio huru na haki, akionya dhidi ya kuenguliwa kwa
wagombea na kuwahimiza wafuasi wa chama hicho kushiriki kwa njia za
kidemokrasia na za amani.
Mhe. Ntobi amesema kuwa licha ya changamoto
zinazoweza kutokea wakati wa kampeni, CHADEMA imejiandaa kushiriki kwa ustarabu
na imeweka wazi kwamba hawatokubali kuvumilia vitendo vya kudhoofisha haki yao
ya kushiriki kikamilifu.
"Baada
ya zoezi la kuengua na kutenguliwa wagombea, tunatarajia kuanza kampeni natoa
kauli hii, sisi CHADEMA tutafanya kampeni za ustarabu sana, haijawahi
kutokea," amesema Ntobi
“Hata
hivyo, tuko tayari kwa aina yoyote ya kampeni ambayo wenzetu wamejipanga
kufanya hatutakuwa tayari kupigwa shavu la kulia tukageuza la kushoto hatutakuwa
tayari kwa hilo, hivyo tunasihi wasiengue wagombea wetu tunaendelea kusihi
tufanye kampeni za ustarabu na za usalama, pia tunahitaji tuwe na uchaguzi
ambao ni wa uhuru, haki, uwazi na ukweli."
"Sisi
tutakuwa wa kwanza kukubali matokeo endapo tutashindwa kwa haki pia tunatoa rai
kwa Chama cha Mapinduzi na dola wakubali matokeo endapo kwenye kitongoji,
kijiji au mtaa atashinda mgombea wa CHADEMA hiyo ndiyo maana ya demokrasia lakini
tukiona uchaguzi si wa haki na uwazi, hatutakubali hatutakubali matokeo hayo ya
kitongoji, kijiji na mtaa."amesema Ntobi
Ntobi pia ametoa wito kuhakikisha kuwa watu
wanaopiga kura ni wakazi halali wa maeneo husika, huku akisisitiza kuwa Novemba
27, siku ya kupiga kura, ni muhimu kuwa na uthibitisho wa utambulisho ili
kuepusha udanganyifu.
"Kwenye
mwongozo wa katiba iliyoandaliwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, inamruhusu
mtu kupiga kura baada ya kutambuliwa na wakazi wa eneo husika kwahiyo, siku ya
kupiga kura tunajukumu la kuwathibiti wanafunzi na watu wengine wasio wakazi wa
eneo husika," amesema.
Ameendelea kufafanua juu ya taratibu za kamati za
rufaa, ambazo zinatakiwa kujumuisha wawakilishi kutoka vyama vyote vya siasa,
akibainisha kuwa mpaka sasa CHADEMA haijapokea taarifa yoyote ya kushiriki
katika kamati hizo huku akionyesha wasiwasi juu ya ukosefu wa mwaliko kwa
CHADEMA kushiriki kwenye kamati za rufaa.
"Kwa
mujibu wa ratiba, leo tarehe 4 mwezi wa 11 ni siku ya uteuzi wa kamati za rufaa
kwenye kata ni lazima aingie mwanasiasa wa chama chochote cha kisiasa katika
kamati hiyo inayoundwa kwa ngazi ya kata na baadaye kwa ngazi ya jimbo,"
amesema Ntobi,
Ntobi amehimiza kuheshimu misingi ya demokrasia na
kusisitiza kuwa CHADEMA itazingatia 4R za Rais pamoja na maadili ya demokrasia.
Ametoa angalizo kuwa chama hicho hakitarajii kuona
vitendo vya kuenguliwa kwa wagombea wake, jambo ambalo linaweza kudhoofisha
misingi ya haki na usawa kwenye uchaguzi huu.
"Kwa
mujibu wa ratiba, leo tarehe 4 Novemba ni siku ya uteuzi wa kamati za rufaa
katika kata kamati hizo zilipaswa kuundwa leo, na ni lazima zishirikishe
mwanasiasa kutoka chama chochote cha siasa”.
Kamati hii inaanzishwa kwa ngazi ya kata na
baadaye kuundwa kwa ngazi ya jimbo hata hivyo, hadi ninavyoongea muda huu,
hatujapokea barua yoyote inayotualika sisi CHADEMA kushiriki kwenye kamati hizo
za rufaa tukizingatia kanuni za 4R za Rais pamoja na misingi ya demokrasia
tunayoheshimu kama chama, hatutarajii kuona kitendo cha kuenguliwa kwa wagombea
wetu," amesema Ntobi.
Viongozi wengine wa chama hicho wamesema wamejipanga
kikamilifu kuhakikisha wanashiriki uchaguzi huo kwa amani, utulivu, na usalama,
huku wakisisitiza haki sawa katika kila hatua ya uchaguzi huo.
Kampeni za uchaguzi huo kwa wagombea zinatarajiwa
kuanza tarehe 20 hadi 26 Novemba, huku uchaguzi wa serikali za mitaa ukipangwa
kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.