Na Mapuli Kitina Misalaba
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Serengeti leo kimeibua
malalamiko baada ya kudai kuwa wagombea wake kwa asilimia 90 walioomba nafasi
katika uchaguzi wa serikali za mitaa wameenguliwa katika mikoa ya Shinyanga,
Simiyu, na Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11,
2024, katika ofisi za kanda hiyo, Katibu wa CHADEMA kanda ya Serengeti Jackson
Mnyawami, amesema kuwa wagombea wa CHADEMA wamekuwa wakikumbana na changamoto
mbalimbali katika mchakato wa uchaguzi, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya
wagombea chama hicho katika kila mtaa wameenguliwa.
Mnyawami ameeleza kuwa chama kimekuwa kikitekeleza
majukumu yake kwa kufuata kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa za mwaka huu,
lakini licha ya jitihada hizo, wagombea wake wengi wameondolewa, huku baadhi ya
wagombea waliopitishwa wakikumbana na pingamizi.
“Watanzania
kama ambavyo mnafahamu tulianza uteuzi wa wagombea ikiwemo jimbo la Shinyanga
mjini na majimbo mengine ya kanda ya Serengeti ambayo inamajimbo 24 na Mikoa 3 na
baadhi ya wagombea wetu waliteuliwa na kuna mamia ya mamia kama siyo maelfu ya
wagombea wetu wajateuliwa katika mchakato huu, na kama mnavyofahamu uchaguzi
unaendeshwa kwa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa za 2024, mpaka sasa
asilimia 90 ya wagombea wetu mpaka 95 walioenguliwa hawajaenguliwa kwa sababu
za kikanuni lakini kama haitoshi hata wale ambao waliteuliwa wamewekewa
pingamizi kinyume na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa”amesema
Mnyawami
CHADEMA imechukua hatua za kukata rufaa juu ya
uamuzi huo na kueleza kuwa timu za kanda zimepelekwa maeneo ya Maswa, Bariadi,
Itilima, na Serengeti kusaidia wagombea wake kuandaa rufaa.
Mnyawami amesisitiza kuwa licha ya changamoto
zinazowakumba, chama hicho kimejizatiti kufuata taratibu zote za kikanuni ili
kuhakikisha haki inatendeka.
Mnyawami pia ametoa wito kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuwarudisha wagombea wa
CHADEMA na vyama vingine waliotimuliwa na kuwaruhusu kushiriki kikamilifu
katika uchaguzi ujao ili wananchi waweze kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Leo
tuna timu imeenda Maswa, kuna timu Imeenda Bariadi, Kuna timu imeenda Itilima,
kuna timu imeenda jimbo la Serengeti kusaidia na tupo hapa kwenye awamu ya
kuandika rufaa pamoja na mizengwe yote ambayo inafanyika hatutakata tama
kufuata taratibu zote za kikanuni kuhakikisha wagombea wetu wote wanaandika
rufaa na wanaziwasilisha kwa mwenyekiti wa kamati ya rufaa”
“Pamoja
na kufuata hatua zote tunamtaka waziri wa TAMISEMI Nchengelwa kuwarejesha
wagombea wa CHADEMA na vyama vingine wote warudi twende kwa wananchi tukaombe
kura na wananchi wapate fursa ya kuchangua viongozi wanaowataka”. Amesema
Mnyawami
Kwa upande wake, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa
Shinyanga, Agatha Mamunya, pamoja na Katibu wa CHADEMA jimbo la Shinyanga
mjini, Sebastian Polepole, wameunga mkono hoja hiyo, wakisisitiza umuhimu wa
wagombea walioenguliwa kurejeshwa.
CHADEMA wamedai kuwa utaratibu unaotumika kuwaengua
wagombea hao si wa haki, ambapo wameisisitiza serikali kuheshimu misingi ya
kidemokrasia kwa kutoa nafasi kwa wagombea wote kuwania nafasi walizoomba.
Misalaba Media, imezungumza na baadhi ya wagombea wa
CHADEMA walioenguliwa wameeleza kusikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa katika
kinyang’anyiro hicho.
Wamesema kuwa uamuzi huo unaenda kinyume na kanuni
za uchaguzi na kuiomba serikali kuwaangalia kwa haki na kurudisha majina yao
ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Novemba 27, 2024.
Misalaba Media inaendelea kuwasiliana na wahusika ili kupata ufafanuzi zaidi kuhusu madai ya kuenguliwa kwa wagombea hao.