Na Mapuli Kitina Misalaba
Katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye
uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024,
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia Mkurugenzi wake, Dkt. Kalekwa
Kasanga, imeandaa bonanza la michezo mbalimbali ambalo limefanyika katika kata
ya Tinde.
Bonanza hilo limejumuisha michezo kama mbio za
baiskeli kwa wanawake na wanaume, kukimbiza kuku, mbio za magunia, na kuvuta
kamba kwa wanawake na wanaume ambapo washindi wa michezo wamezawadiwa, huku
wasanii wa nyimbo za asili wakitumbuiza kwa nyimbo zenye ujumbe wa kuhamasisha
ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mgeni rasmi katika bonanza hilo ni Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ambaye pamoja na mambo mengine amewahimiza
wananchi kujitokeza kwa wingi katika kampeni za wagombea na siku ya uchaguzi
ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuchagua viongozi wa vijiji na
vitongoji vyao.
“Tuna
zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa tarehe 27 mwezi huu, ambapo zimebaki
siku chache kuanzia tarehe 20, wagombea wataanza kampeni hadi tarehe 26, kwa
hiyo tujitokeze tukawasikilize wagombea, na tarehe 27 tujitokeze tukapige
kura.”amesema Wakili Mtatiro
Amesisitiza kuwa kuchagua viongozi wa vijiji na
vitongoji ni muhimu, kwani wenyeviti hao wana majukumu makubwa yanayohusu
masuala mbalimbali, ikiwemo ardhi na changamoto za kijamii na kwamba amewataka
wananchi wakiwemo vijana, wazee na wanawake, kufahamu umuhimu wa kupiga kura
kwa kuwa viongozi wanaowachagua watakuwa msaada mkubwa katika utatuzi wa
changamoto zinazowakabili.
“Kati
ya mambo muhimu ambayo unaweza kufanya duniani ni kutokwenda kupiga kura na
kuwachagua viongozi wako kuna wenyeviti wa vitongoji na vijiji ambao
tunawahitaji sana, kwani wana mamlaka juu ya masuala yako muhimu kama ardhi na
changamoto mbalimbali pakitokea shida na huna mwenyekiti wa kijiji, wewe ndiye
utakayepata tabu kwa hiyo niwaombe vijana, wazee, na akina mama, tarehe 27
mwezi huu wa Novemba, ambayo ni siku ya Jumatano, twende tukapange foleni na
tupige kura kuwachagua viongozi wetu wa vijiji na vitongoji.”amesema
Wakili Mtatiro
Wakili Mtatiro ameendelea kusisitiza kwamba serikali
ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, inafanya juhudi kubwa kutatua matatizo ya wananchi ambapo amewahimiza
wakazi wa kata ya Tinde kuwa huru kuwasiliana naye kuhusu changamoto zao bila
kusubiri mikutano ya hadhara.
“Serikali
ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Samia Suluhu Hassan, kazi yake kubwa hapa Shinyanga ni kutatua matatizo
yanayoikabili jamii na wananchi. Kwa hiyo, mimi nipo kuwaomba wananchi muwe
huru kuwasiliana na mimi muda wote hasa pale kunapokuwa na changamoto;
tusisubiri hadi mikutano ya hadhara ndipo tueleze changamoto za miezi miwili au
mitatu zilizopita.”Amesema Wakili Mtatiro
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Tinde, Mhe.
Jafary Makwaya, amempongeza Dkt. Kalekwa Kasanga kwa kuandaa bonanza hilo,
ambapo amesema litasaidia kuongeza uelewa na hamasa kwa wananchi kuhusu umuhimu
wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Aidha amesema bonanza hilo limekuwa fursa nzuri ya
kuwakutanisha wananchi, kuwaburudisha na kuwaelimisha kuhusu uchaguzi.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Tinde wamepongeza juhudi
za serikali katika kuandaa bonanza hilo, wakisema kuwa michezo na burudani
zilizofanyika zimeongeza mshikamano katika jamii.
Wameahidi kujitokeza kwenye kampeni za wagombea na siku ya uchaguzi ili kumpata kiongozi anayefaa na kujenga mustakabali bora wa vijiji na vitongoji vyao.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili
Julius Mtatiro, akizungumza kwenye bonanza hilo leo Novemba 14, 2024.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili
Julius Mtatiro, akizungumza kwenye bonanza hilo leo Novemba 14, 2024.
Diwani wa kata ya Tinde Mhe. Jafary Makwaya, akizungumza
kwenye bonanza hilo leo Novemba 14, 2024.
Wakazi wa kata ya Tinde wakiwa kwenye bonanza la
michezo mbalimbali ambalo limeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
kupitia mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Kalekwa Kasanga kwa lengo la
kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Wakazi wa kata ya Tinde wakiwa kwenye bonanza la michezo mbalimbali ambalo limeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Kalekwa Kasanga kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Wakazi wa kata ya Tinde wakiwa kwenye bonanza la michezo mbalimbali ambalo limeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Kalekwa Kasanga kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.