JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI TANZANIA LAELEZA NAMNA UJENZI HOLELA UNAVYOATHIRI UTOAJI HUDUMA ZA DHARURA.













……….

Happy Lazaro, Arusha

Arusha .JESHI la Zimamoto na Uokoaji Tanzania limeeleza namna ujenzi holela katika maeneo mengi ya makazi unavyoleta changamoto kubwa katika kutoa huduma za dharura, hasa wakati wa matukio ya moto na majanga mengine yanayosababisha maafa.

Hayo yamebainishwa mkoani Arusha na Kamishna wa jeshi la Zima moto na Uokozi CGF John Masunga wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza dogo la wafanyakazi linalofanyika katika hotel ya Lush Garden nje kidogo ya jiji la Arusha.

CGF Masunga alisisitiza kuwa jenzi usiozingatia miundombinu bora ya barabara, unafanya iwe vigumu kwa magari ya zimamoto kufika kwa haraka kwenye maeneo ya dharura na hivyo kusababisha athari kubwa kwa eneo husika.

“Hali hii inahatarisha usalama wa wananchi na kuongeza athari za majanga kwa ujumla. Jeshi hilo linashauri ujenzi wa mipango miji inayozingatia miundombinu ya dharura ili kuhakikisha usalama wa jamii katika matukio ya dharura”amesema Masunga.

Hata hivyo amesema kuwa jeshi hilo la Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi jeshi hilo limefanikiwa kujenga vituo 80 katika mikoa yote Nchini.

“Kati ya vituo hivyo 56 vipo katika ngazi ya wilaya na 24 viko kwenye viwanja vya ndege ,pia jeshi hilo lina ofisi 73 za kutoa elimu ya kinga na tahadhali ya majanga ya moto katika wilaya mbali mbali na vituo 7 vya kutoa huduma mpakani “. amesema.

Aidha amesema jeshi hilo linauhitaji wa vituo vipya 237 katika wilaya na maeneo mengine ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi na jitihada za kusogeza huduma za Zimamoto na Uokoaji katika maeneo mbalimbali bado zinaendelea.

Amesema katika kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha 2024/25 jeshi hilo linampango wa kujenga vituo 7 vitakavyosaidia kuboresha shughuli za jeshi la zimamoto na Uokoaji hapa nchini.

“Katika kuimarisha shughuli za zima moto na uokoaji ,tumefanikiwa kununua magari 12 ya zima moto na kati ya hayo mawili yanauwezo wa kuzima moto kwenye majengo marefu”

Ameongeza kuwa ,serikali imekamilisha upatikanaji wa mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 100 kutoka taasisi ya Falme za kiarabu kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali ikiwemo magari 150 ya kuzima moto.

Naye katibu Mkuu wizara ya Mambo ya Ndani,Ally Gugu amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na jeshi hilo la Zimamoto na Uokoaji, licha ya changamoto zinawakabili na kusema serikali inachukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizo ili kuboresha shughuli za utendaji kazi wa jeshi hilo ili kuiweka nchi salama na wananchi wake .

“Serikali inatambua mchango wenu na sisi kama wizara tutahakikisha tunashugulikia changamoto zenu”amesema.

Aidha ametoa rai kwa miji na majiji hapa nchini ikiwemo jiji la Arusha kuhakikisha wanasimamia wananchi kujenga makazi yao kwa kuzingatia mipango miji ili kuifanya miundombinu ya barabara inapitika kirahisi.
Previous Post Next Post