Akizungumza katika Kongamano la Fursa za Kiuchumi kwa Vijana Mkoani Mara Wilaya ya Tarime lililofanyika tarehe 14 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa CMG, Mbunge wa Viti Maalum Vijana Tanzania, Mhe. Juliana Didas Masaburi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu ina Mifuko zaidi ya 71 yenye fursa za kuwawezesha vijana lakini haiwafikii walengwa ipasavyo.
Kongamano hilo lilijumuisha Vijana zaidi ya 1,000 kutoka Wilaya zote Saba za Mkoa wa Mara na Mikoa ya jirani ambapoo vijana walipata mafunzo kutoka kwa Wakufunzi na Wataalam wa Wizara ya Madini, Wizara ya Nishati, Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi kadhaa
"Tutakuwa viongozi waongo tukiwaambia kuwa Serikali ya CCM au Serikali ya Awamu ya Sita itawaletea fedha mifukoni mwenu vijana kila siku au kila mwisho wa mwezi. Lakini Serikali ya CCM chini ya Mama Samia imewaletea vijana fursa na jukumu letu viongozi ni kuwaletea fursa ili mzione, mjipime nani anaweza kufanya nini, nani anaweza kufanya wapi, nani anatakiwa kwenda wapi" - Mhe. Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum Vijana Tanzania
"Fursa ambazo Serikali imetenga kwaajili ya vijana ni nyingi sana. Ofisi ya Waziri Mkuu ina mifuko ya kuwezesha vijana lakini vijana hawajui ni wapi na kwa namna gani wataweza kuifikia ile mifuko ili wanufaike" Amesema, Juliana Masaburi
"Mifuko ya kuwezesha vijana ipo Makao Makuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, huwezi kumtoa kijana Tarime (Nyamongo) kwenda Dodoma kutambua kuna fursa gani. Kutoka Tarime-Dodoma nauli si chini ya Tsh. 60,000. Kwa vipato vya vijana hawataweza kuzifuata hizo fursa Dodoma" - Juliana Masaburi
"Tunaishauri Serikali angalau ifungue Ofisi mikoani Mahususi kwaajili ya vijana ili wajue faida na fursa ya mifuko ya kuwawezesha vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mtakuwa mmewasaidia sana vijana" - Juliana Masaburi
Juliana Masaburi amewashauri vijana kuwa, Badala ya kijana kuweka Tsh. 10,000 akafanya michezo ya kubashiri ikapotea/ikaliwa ni afadhali kijana huyu atumie hiyo fedha kuingia kwenye tovuti ya Waziri Mkuu ili apate faida zaidi ya kujifunza fursa zilizopo
"Tunaomba mifuko ya kuwezesha vijana kitaifa iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu iwe rafiki na iwe Mahususi kwa vijana na iwafikie vijana kiukweli. Mifuko ipo zaidi ya 71 lakini hakuna hata kijana mmoja hapa ambaye amenufaika na Mfuko mmoja" Ameongeza Juliana Masaburi
Juliana Masaburi amesema, Mheshimiwa Rais Samia anajitahidi kupeleka bajeti kubwa kwa vijana lakini kuna kitu hapa katikati hakijakaa sawa ili hizi fursa ziwafikie walengwa ambao ni vijana
"Kuna fursa zisizo rasmi, naomba vijana twende tukazifuate maana tumeambiwa sehemu ya kuzifikia, tusikae tu tunaongea ajira hakuna lakini ajira zipo za kujiajiri hasa sisi wenyewe. Twende tukachukue mikopo lakini tuwe waaminifu kurudisha ili vikundi vingine kupata" - Juliana Masaburi
Pamoja na mambo mengine, Juliana Masaburi amewasisitiza watu wote waliojumuika katika Kongamano la Fursa za Kiuchumi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Mwisho, Juliana Masaburi amemshukuru Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa WIlaya, Wabunge wa Viti Maalum, Viongozi wa CCM & UVCCM Mkoa wa Mara, Wakufunzi/Wataalamu na Vijana wote waliojitokeza kushiriki Kongamano.