KAMPENI ZA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA ZAFUNGWA RASMI MTAA WA NYASHIMBI KAHAMA

Chama cha Mapinduzi CCM chahitimisha kampeni zake katika mtaa wa Nyashimbi Kahama, wananchi wasisitizwa kudumisha amani utulivu waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni hata katika zoezi la kupiga kura.

Kampeni hizo zimehitimishwa na katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM wilaya ya Kahama Joachim Simbila, ambapo amewataka wanachama wa CCM na wasiokuwa wanachama kukichagua chama cha mapinduzi kwa mustakabali wa maendeleo yao na vizazi vijavyo.

Simbila amewasihi wananchi wenye sifa za kupiga kura kuhakikisha wanaamka asubuhi na mapema ili kuwahi katika vituo vya kupigia kura walipojiandikisha na kila mmoja ahakikishe jirani yake anapiga kura na kukichagua chama hicho.

“Niwaombe sana wana Nyashimbi, siku ya kupiga kura ni kesho Novemba 27, 2024, naomba kwanza muamke asubuhi na mapema muende mkakichague chama cha mapinduzi. Na nitasema kwa nini tunataka mkakichague chama cha mapinduzi, ni kwa sababu ndicho chenye serikali, Rais anatokana na chama cha Mapinduzi, wabunge ni wa chama cha mapinduzi, na madiwani ni wa chama cha mapinduzi”Alisema Simbila

“Na tunapoizungumzia serikali maana yake ndiyo yenye fedha za maendeleo, kwa hiyo si vyema mkaweka mtu ambaye hana serikali kwa sababu utekelezaji wa majukumu yote iwe ni umeme, maji, barabara, afya  au elimu inatokana na fedha zinazoletwa na serikali yetu, niwasihi na niwaombe sana wananchi wenzangu wa mtaa huu wa Nyashimbi mtuchagulieni Chama cha Mapinduzi” Alisisitiza Simbila

Kwa mujibu wa Simbila, chama cha mapinduzi historia yake inatokana na ukombozi wan chi hii kutoka kwenye mikono ya wakoloni.

 “Chama cha mapinduzi historia yake inatokana na ukombozi wa nchi hii kutoka kwenye mikono ya wakoloni, kwa hiyo chama cha mapinduzi ndicho chenye uchungu wa dhati kwa wananchi wake, na ndio maana mnaona huduma nyingine zinaendelea kutekelezwa kwa sababu ya uchungu huo” Alisema

“Nandio maana mnaona huduma nyingine zote zinaendelea kutekelezwa kwa sababu ya uchungu huo,  lakini kwa sababu za kidemokrasia na mashinikizo ya mataifa, ndio maana vikawepo na vyama vingine vya upinzani, lakini nataka niwaambie vyama hivyo haviwezi kuwa na uchungu kama ilivyo chama cha mapinduzi kwa sababu ya historia yake ya kuwakomboa watanganyika kutoka kwenye mikono ya wakoloni” Alisema Simbila

Katika hatua nyingine amewasihi wananchi kupiga kura kwa kufuata utaratibu uliowekwa bila kuathiri amani na utulivu wan chi uliopo ili kuwapata viongozi bora watakaowaletea maendeleo, na kwamba chama sahihi kitakachowaletea maendeleo ni Chama Cha Mapinduzi CCM.

MWISHO

 

 

Previous Post Next Post