Na Mapuli Kitina Misalaba
Usiku wa
kuamkia leo, wananchi wa Kata ya Bubiki Wilaya ya Kishapu walifanikiwa kukamata
roli lililokuwa likitorosha mifuko 107 ya mbegu za pamba kutoka kwenye Chama
cha Ushirika (AMCOS) cha eneo hilo leo Novemba 15, 2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, amefika eneo la tukio mapema asubuhi baada ya kupokea taarifa za kukamatwa kwa roli hilo huku akielezea hatua zilizochukuliwa na serikali.
Mkude ameongeza kuwa ukaguzi uliofanyika kwenye
ghala la AMCOS ulibaini kuwepo kwa mifuko 443 ya mbegu, huku stakabadhi
zikionyesha kuwa AMCOS hiyo ilikuwa imepokea jumla ya mifuko 550 na kwamba mifuko
107 iliyokamatwa inadaiwa kuwa sehemu ya mbegu hizo.
“Usiku wa kuamkia leo, wananchi wa Kata ya Bubiki walifanikiwa kuwakamata
watu waliokuwa wakitorosha mbegu za pamba kutoka kwenye AMCOS ya Bubiki wakiwa
njiani kuelekea Mwanza. Nilipata taarifa hizo asubuhi, na nilifika eneo la
tukio mapema na kukuta roli lililokuwa limebeba mifuko takribani 107 ya mbegu
za pamba. Hata hivyo, dereva na tingo wake walitoroka na kuacha roli hilo bila
ufunguo.”
“Niliporudi kwenye AMCOS ya Bubiki, tulikuta mifuko 443 ya mbegu za pamba
ikiwa imebaki kwenye ghala.”ameseme DC Mkude
“Tulipouliza taarifa za upokeaji wa mbegu hizo, tulipatiwa stakabadhi
(invoice) iliyoonyesha kuwa AMCOS hiyo ilipokea mifuko 550. Hii inathibitisha
wazi kwamba mifuko 107 iliyokamatwa ilitoka kwenye AMCOS hiyo ya Bubiki.
Uchunguzi ulionyesha kwamba ghala halikuvunjwa, na ufunguo wa ghala ulikuwa
mikononi mwa kaimu mwenyekiti wa AMCOS. Tulimwomba kufungua ghala hilo, na
tukathibitisha kuwa mifuko 443 ilikuwa bado ipo ndani.”amesema
DC Mkude
Katika uchunguzi zaidi, mkuu huyo wa wilaya amesema
kuwa wahusika wanne wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku mmoja akitoroka
ambapo ameeleza kuwa mifuko iliyobaki imegawiwa kwa wakulima ili kuhakikisha
wanapata mbegu kwa wakati:
“Baada ya hapo, tulichukua hatua za kuwakamata wahusika wanne wa tukio
hili. Hata hivyo, mmoja wao alitoroka. Tulirudi na watuhumiwa wanne ili hatua
za kisheria zichukuliwe. Kabla ya kufanya hivyo, tulihakikisha mifuko 443
iliyobaki inagawiwa kwa wakulima kwa uwazi. AMCOS hiyo iliandika hati ya
kukabidhi mbegu hizo kwa viongozi wa kijiji, mtendaji wa kijiji, na diwani wa
eneo hilo, na ugawaji ulianza mara moja ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu
kwa wakati kwa ajili ya msimu wa kilimo cha pamba.”
“Kuhusu roli hilo, hatukuweza kuliondoa eneo la tukio hadi mchana kwa
sababu hatukupata funguo zake. Dereva alikimbia na funguo halisi. Kwa sasa,
roli hilo lipo mikononi mwa polisi, nikiwa nimeagiza lifikishwe kituoni Kishapu
pamoja na mali iliyokuwa kwenye roli hilo ili hatua zaidi zichukuliwe.”amesema DC Mkude
Aidha, ametoa wito kwa AMCOS nyingine kuchukua
tahadhari na kuhakikisha usimamizi mzuri wa mbegu za pamba, huku akiahidi
kuendeleza ukaguzi katika vyama vingine vya ushirika.
“Natoa wito kwa AMCOS nyingine zote kuhakikisha kuwa zinatoa taarifa
sahihi za mbegu za pamba wanazopokea na kusambaza. Nitafanya ukaguzi wa AMCOS
zote zinazopokea mbegu za pamba ili kubaini kama mbegu zinawafikia wakulima
kama ilivyopangwa. Pia, nawasihi wakulima kushirikiana na serikali kama
walivyofanya wananchi wa Kata ya Bubiki, ambao walihakikisha mbegu hizo
hazitoroshwi. Ushirikiano wao ni wa kupongezwa.”amesema
DC Mkude
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha,
amesema kuwa serikali ya mkoa inachukua hatua kuhakikisha wahusika
wanawajibishwa:
Macha ameongeza kuwa serikali inahamasisha wakulima
kufuata maelekezo ya wataalam ili kuongeza tija katika zao la pamba ambapo
ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wakulima kuwa hatua kali zitachukuliwa
dhidi ya wale wanaojihusisha na vitendo vya wizi na utoroshaji wa rasilimali za
wakulima.
"Taarifa hizi nimezipata kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,
zikihusu kukamatwa kwa mbegu za pamba ambazo zinashukiwa kuibiwa au kutolewa
kwa njia isiyo sahihi. Kwa sasa, tunachosisitiza ni kuhakikisha kwamba sheria
inachukua mkondo wake."
"Natoa rai kwa wakulima wote kufuata maelekezo
yanayotolewa na wataalam. Kwa bahati nzuri, nilifanya ziara katika maeneo hayo
nikiwa na Balozi wa Pamba, na tulitoa maelekezo mahsusi kuhusu mambo
yanayopaswa kuzingatiwa ili kufanikisha uzalishaji bora wa zao la pamba."amesema
RC Macha
"Kwa wale wanaotafuta utajiri wa haraka kwa kutorosha mbegu za
pamba, nawatahadharisha kuacha mara moja. Hilo ni kosa kubwa la kihalifu, na
tunapowakamata, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Kuhusu suala la mtuhumiwa
aliyekamatwa na mbegu hizi, nitalifuatilia kwa karibu kuanzia leo hadi pale
hatua za kisheria zitakapochukuliwa na adhabu kutolewa. Hii itakuwa fundisho
kwa wengine wenye nia ya kuendeleza vitendo kama hivyo."amesema
RC Macha
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Bubiki wametajwa kuwa
mstari wa mbele katika kufanikisha operesheni hiyo ambapo walihakikisha roli
hilo haliondoki usiku kwa kuweka mitego baada ya kupata taarifa za wizi wa
mbegu.
Wananchi hao wameomba serikali kuimarisha ulinzi na
kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake ili kulinda rasilimali za wakulima.
MISALABA MEDIA itaendelea kufuatilia maendeleo ya tukio hilo, ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa na matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya dola.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, upande
wa kushoto akionyesha mifuko ya Mbegu za Pamba zilizokamatwa leo Novemba 15,
2024