MAELEKEZO YA RAIS SAMIA YAANZA KUTEKELEZWA KATAVI

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amekabidhi jumla ya Hati za Hakimiliki za kimila 691 kwa wanachi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro vilivyopo kata ya Kasansa katika halmashauri ya Mpimbe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika tarehe 21 Novemba 2024 katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kasansa wilayani Mlele na kuhudhuriwa na wataalam wa Ardhi kutoka ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Katavi.

Naibu Waziri Pinda amesema kuwa, hatua ya kukabidhi hati hizo ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupima ardhi ya nchi nzima.

"Hizi zote ni juhudi za Mama Samia Suluhu Hassan, anataka nchi nzima hii ipimwe, watu wake wawe na hivi vibali vya ardhi yao" amesema Naibu Waziri Pinda.

Mhe. Pinda ameeleza kuwa, vijiji vya Ntilili na Igalukiro vimenufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia ufadhili wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira iliyowezesha uandaaji wa hati za kimila 691.

"Kupita mradi huu, Ofisi ya Makamu wa Rais imetufadhili tupime vijiji vinavoambatana na Mradi wake hapa juu (Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Uhifadhi wa Banowai) kwa hiyo wanufaika ni Ntilili na Igalukiro ambapo tumayarisha hati 691 zote zipo hapa" ameongeza Mhe Pinda.

Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Katavi Bw. Chediel Mrutu amewaasa wanakijiji hao kuhifadhi hati hizo sehemu salama kwani zikiharibika si rahisi kupata nakala Mbadala.

"Hizi hati ukiweka kwenye eneo ambalo linavuja itaharibika na ikiharibika siyo rahisi kupata nakala yake"

"Zamani watu walikuwa wanafanya lamination, hii hairuhusiwi, tafuta kibegi cha zuri na salama iweke na itunze" amesema Kamishina Mrutu.

Naye Afisa Mipangomiji Mkoa wa Katavi Bw. Flavian Masore kupitia taarifa yake ya mpango wa matumizi bora ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe amesema, mpango huo umewezesha utoaji elimu ya ardhi sambamba na kutenga maeneo muhimu kwa ajili ya matumizi ya bora ya ardhi pamoja na kuandaa hati za ardhi.

"Vijiji vimewezeshwa kutenga maeneo ya matumizi mbalimbali ya kilimo, makazi vyanzo vya maji hifadhi za misitu maeneo ya malisho pamoja na kutunga sheria ndogo ndogo za kusimamia maeneo yaliyopangwa".

Kwa upande wao wananchi wa vijiji vilivyonufaika na hati hizo kupitia kwa wenzao Bi. Joyce Mataluma na Bw. Robert Kasale wamefurahishwa na zoezi zima la utoaji hati milki ambapo wameahidi kuzitunza vizuri.

Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi na Uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila katika halmashauri ya Mpimbwe unaowezeshwa na Tume ya Taifa ya Matumizi bora ya Ardhi kwa ufadhili wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kupitia Mradi wa urejeshwaji endelevu wa Mazingira na uhifadhi wa banowai umewezesha kuandaliwa jumla hati miliki za kimila 691 ambapo kijiji cha Igalukiro zimeandaliwa hati 277 na Ntilili zimeandaliwa hati 414.

Aidha, vijiji hivyo kupitia mradi huo vimepatiwa daftari la usajili la kijiji, cheti cha ardhi cha kijiji, ripoti maalumu ya matumizi bora ya ardhi, ramani ya mipaka ya kila kijiji pamoja na mhuri wa moto kwa ajili ya kusaidia kijiji kutoa hati kwa watu wasio na hati.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi mhe. Geophrey Pinsa (wa pili kushoto) akimkabidhi Hati ya Hakimilki ya Kimila kwa mwananchi wakati wa kukabidhi hati hizo kwa wanachi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
Sehemu ya akina mama waliohudhuria hafla ya kukabidhi Hati ya Hakimilki ya Kimila kwa mwananchi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro katika halmashauri ya Mpimbe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kavuu katika mkoa wa Katavi mhe. Geophrey Pinsa akizungumza wakati wa kukabidhi Hati ya Hakimiliki za Kimila kwa wanachi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro katika halmashauri ya Mpimbe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Previous Post Next Post